Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizindua Kituo cha Mawasiliano kwa Wateja cha Wizara ya Ardhi leo tarehe 7 Januari 2022 jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Mary Makondo. Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akipata maelezo kutoka kwa Afisa Ardhi David Malisa kuhusiana na namna ya Kituo cha Mawasiliano kwa Wateja cha Wizara ya Ardhi kinavyopokea malalamiko ya Wateja alipokizindua leo tarehe 7 Januari 2022 jijini Dodoma. Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akifuatilia upokeaji malalamiko ya wananchi kwenye kituo cha Mawasiliano kwa Wateja cha Wizara ya Ardhi mara baada ya kukizindua leo tarehe 7 Januari 2022 jijini Dodoma. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Mary Makondo. Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiangalia ndege ya kuchukua picha za anga (Drons) kwa ajili ya uandaaji ramani za msingi za upimaji leo tarehe 7 Januari 2022 jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Mary Makondo.

********************************

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imezindua kituo cha Mawasiliano kwa Wateja kwa lengo la kuondoa kero za wananchi katika masuala ya ardhi.

Uzinduzi wa kituo hicho umefanywa leo tarehe 7 Januari 2022 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika ofisi za Wizara zilizopo Mtumba jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho, Waziri Lukuvi alisema, kwa kutumia maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano na habari yaliyopo sasa wizara yake imeona zipo baadhi ya huduma za ardhi zinazoweza kutolewa kwa njia ya simu na mitandao ya kijamii ambazo hazimlazimu mwananchi kufika ofisi za ardhi.

‘’Wizara imeanzisha kituo cha Mawasiliano kwa Wateja kitakachotoa huduma ya mawasiliano moja kwa moja na mwananchi kwa kutumia simu na ujumbe wa maneno kupitia Whatsup ambapo majibu au ufafanuzi utatolewa kwa wananchi na wataalamu wa ardhi’ alisema Lukuvi

Kwa mujibu wa Lukuvi, Kituo hicho cha Mawasiliano kwa Wateja kina wataalamu wabobezi katika masuala ya ardhi waliopata mafunzo yakinifu ya kuifanya kazi ya kutoa huduma kwa wateja kwa weledi na kutoa majibu kwa wakati.

Aidha, Waziri Lukuvi alitumia fursa ya uzinduzi wa kituo hicho kuwataka wananchi kukitumia kituo cha Mawasiliano kwa Wateja cha Wizara ya Ardhi kuwasilisha kero mbalimbali zikiwemo za matapeli wa ardhi, watumishi wa sekta ya ardhi wasio waaminifu pamoja na wale madalali wanaochukua fedha za wapangaji na kusisitiza kuwa, anayepaswa kutoa fedha kwa madalali ni mwenye nyumba na siyo mpangaji.

Aliongeza kwa kusema, kupitia kituo hicho mwananchi atalazimika kupiga simu na kuongea moja kwa moja na watoa huduma kupitia namba 0739-646-885 au kutuma ujumbe wa maneno kupitia mtandao wa Whatsup kwa namba hizo. Kituo hicho kitakuwa wazi siku za kazi kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri kwa ajili ya kutoia huduma kwa wananchi.

‘’Ni matumaini yangu kituo hiki kitatoa fursa kwa wananchi kupata huduma za ardhi kwa haraka, kwa ufanisi na kwa gharama nafuu kwa kuwa mwananchi hatakazimika kufika ofisi za ardhi endapo huduma anayohitaji anaweza kuipata kupitia simu.

Alitoa rai kwa wananchi kukitumia kituo hicho kwa kupiga simu na kutuma ujumbe wa maneno kupitia namba ya simu iliyotangazwa na kutumia tovuti ya wizara kupata huduma kwa urahisi bila usumbufu ili kuepuka gharama za kusafiri sambamba na kutumia muda mwingi kufuata huduma hizo ofisi za wizara makao makuu, ofisi za ardhi za mikoa na halmashauri.

Uanzishwaji Kituo cha Mawasiliano kwa Wateja ni moja ya mikakati mbalimbali ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhakikisdha huduma kwa wateja wa ardhi zinaboreshwa na zionatolewa kwa weledi na ufanisi mkubwa.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: