Katibu Mkuu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara (Kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) Mhe. Wamkele Mene walipokutana pamoja na kufanya mazungumzo Januari 24, 2022 katika Ofisi za Makao Makuu ya Sekretarieti hiyo yaliyopo Accra, nchini Ghana.

........................................................................

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika AfCFTA, Sekta Binafsi na Wadau wengine nchini kuwaelimisha wananchi kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana katika Eneo hilo.

Katibu Mkuu ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya AfCFTA Mhe. Wamkele Mene Januari 24, 2022 katika Ofisi za Makao Makuu ya Sekretarieti hiyo yaliyopo Accra, nchini Ghana.

Pamoja na mambo mengine yaliyojiri katika mazungumzo hayo, Prof. Kahyarara alimpongeza Mhe. Wamkele kwa hatua nzuri iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mkataba wa AfCFTA na kusisitiza utayari wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kushiriki kikamilifu katika kutekeleza Mkataba huo.

Naye Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya AfCFTA Mhe. Wamkele Mene aliipongeza Tanzania kwa kuwasilisha Hati ya kuridhia mkataba wa AfCFTA kwenye Kamisheni ya Umoja wa Afrika na kuwa nchi ya 40 kati ya nchi 55 za Afrika kufanya hivyo na alitoa wito kwa Watanzania wenye vigezo stahiki kuchangamkia fursa za kazi zinazoendelea kutangazwa na Sekretarieti ya AfCFTA.

Aidha , Viongozi hao walikubaliana kuendelea kushirikiana katika masuala yanayohusu Mtangamano wa Afrika kupitia Mkataba wa AfCFTA hususani katika kukuza uwekezaji katika Sekta ya Usafirishaji na Uwezeshaji Biashara, Uongezaji thamani mazao ya kilimo na uzalishaji madawa

Katibu Mkuu, Prof. Godius Kahyarara yupo nchini Ghana kushiriki Mkutano wa 10 wa Maafisa Waandamizi wa Biashara wa Afrika unaofanyika Accra, Ghana kuanzia tarehe 24-27 Januari 2022. Mkutano huo utafuatiwa na Mkutano wa Nane (8) wa Baraza la Mawaziri wa Biashara wa Afrika utakaofanyika kuanzia tarehe 28-29 Januari 2022.

Prof. Godius Kahyarara, Katibu Mkuu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara (Kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Wamkele Mene, Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA).
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: