Naibu Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya na Diwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Mhandisi Maryprisvca Mahundi amewataka wanawake wa Wilaya ya Chunya kujifunza kwa wengine ili wamiliki uchumi wao badala ya kuwategemea wanaume.


Ameyasema hayo katika sherehe ya usiku wa mwanamke iliyofanyika Chunya Mjini kwa lengo la kujifunza ujasiriamali,afya na changizo la nyumba kwa ajili ya Katibu wa Umoja wa Wanawake(UWT)Wilaya ya Chunya.


Mahundi amesema endapo wanawake watafanikiwa kumiliki uchumi wao watawasaidia wanaume kusomesha watoto pia kusaidia ujenzi wa nyumba bora.


Amehimiza wanawake kwenda mikoa mingine kujifunza na kubadilishana uzoefu badala ya kubweteka mahala pamoja na kufanya shughuli zisizo na tija.


Akiunga mkono ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UWT Mahundi ameahidi kuchangia shilingi milioni mbili ambapo wadau wengine wamechangia jumla ya shilingi milioni kumi na saba ikiwa ni fedha taslim shilingi milioni tatu.


Pia vifaa mbalimbali vimechangishwa sambamba na mifuko ya saruji ilhali Naibu Spika naye akiwa ameahidi kuchangia mifuko ya saruji.


"Nawaomba tutekeleze ahadi zetu ili nyumba ya Katibu imalizike kwa wakati"alisisitiza Mahundi.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa sherehe Anjela Sompo mbali ya kumshukuru Naibu Waziri wa Maji kuitikia wito pia usiku huo wameutumia kujifunza afya ya uzazi,ujasiriamali na upendo kwa wanawake .

Share To:

Post A Comment: