Na Mwandishi wetu, Simanjiro
SHULE ya msingi ya Bilionea Saniniu Laizer ya Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara na O'Brien ya Kia Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro zimeanzisha ushirikiano rasmi kwa ajili ya maendeleo ya wanafunzi wa maeneo yao.

Mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite, Bilionea Saniniu Laizer ambaye alijenga shule hiyo ya mtaala wa kiingereza na kuikabidhi Serikali amesema ushirikiano huo utanufaisha shule hizo.

Bilionea Laizer amewashukuru viongozi wa shule ya O'Brien kwa kuwapa mhandisi wa kusimamia ujenzi wa bwalo kwa ajili ya kula chakula wanafunzi wa shule hiyo.

"Tunashukuru pia kwa kuwapatia wanafunzi wetu mipira wamefurahi mno na ahadi ya kuwafungia bembea ili wakati wa mapumziko ya masomo wajiburudishe," amesema bilionea Laizer.

Amesema ushirikiano mpya wa shule hizo mbili utasababisha maendeleo makubwa kwa jamii za maeneo hayo kwani hivi sasa mwamko wa elimu umekuwa mkubwa kwao.

"Tupo tayari kwa ushirikiano mpya wa shule hizi mbili kwani lengo letu ni kujifunza na kuhakikisha tunafika mbali zaidi kwenye elimu," amesema bilionea Laizer.

Pia, ameishukuru serikali kwa kuipatia shule hiyo walimu watano japokuwa wanasubiri kupatiwa walimu wengine watano ili wafundishe wanafunzi wao.

Mwalimu mkuu wa shule ya O'Brien, Nimla Mbangu amesema ushirikiano wa shule yao na shule ya Saniniu Laizer, utazidi kufanikisha maendeleo ya pande zote.

Mwalimu Mbangu amempongeza bilionea Laizer kwa namna anavyojitoa kuzisaidia shule zote mbili kwa manufaa ya wanafunzi wa jamii wa maeneo hayo.

"Endelea kuwa na moyo huo huo wa kusaidia jamii ya maeneo haya kwani Mungu amekujalia uwezo mkubwa wa kiuchumi na umesambaza upendo kwa kutumia na jamii inayokuzunguka," amesema.
Share To:

Post A Comment: