Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi.Khadija Mwenda akizungumza na wakaguzi wanaofanya kazi OSHA kutoka maeneo mbalimbali nchini wakati wa hafla za kuhitimisha mafunzo ya siku tano kwa wakaguzi hao yaliyofanyika Mkoani Morogoro kunzianzia Novemba 29 mpaka Desemba 3, 2021.Mkurugenzi wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Alexander Ngata akizungumza na wakaguzi walioshiriki katika mafunzo ya siku tano yaliyofanyika mkoani Mororgoro kwa lengo la kukuza uelewa juu ya mambo mbalimbali ikiwemo uadilifu na miiko ya utumishi wa umma.Wakaguzi wa OSHA wakikwa katika majadiliano na muwezeshaji wa mafunzo (hayupo pichani) juu ya nmna bora ya kuboresha huduma za Ukaguzi wa usalama na afya katika maeneo ya kazi wakati wa kuhitimisha mafunzo ya siku tano kwa wakaguzi hao yaliyofanyika mkoani Morogoro.Mkufunzi Stellah Cosmas akiwafundisha wakaguzi wa OSHA, juu ya kuzingatia maadili wakati wakifanya kazi zao za ukaguzi.

*******************

Na Mwandishi Wetu

Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) wametoa mafunzo ya siku tano kwa wakaguzi wa kada mbalimbali wanaofanya kazi chini ya taasisi hiyo kwa lengo la kuwaongezea weledi katika shughuli zao za ukaguzi ili kuleta tija kwa taifa kwa kuhakikisha maeneo yote ya kazi yanakaguliwa ipasavyo na yanazingatia sheria Na.5 ya mwaka 2003 ya usalama na afya na kanuni zake.

Akifunga mafunzo ya siku 5 yaliofanyika Mkoani Morogoro, Mtendaji Mkuu wa OSHA Bi. Khadija Mwenda amewataka wakaguzi kutoka OSHA kuendelea kuzingatia uadilifu,tunu za taasisi na miiko ya utumishi wa umma wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.

“Dira yetu inataka maeneo yote ya kazi yawe salama na yenye afya, hivyo tutahakikisha tunawakagua na kuwashauri wadau wetu waweze kukidhi matakwa ya sheria ya usalama na afya mahali pa kazi, kupitia mafunzo haya tume kumbushana namna ambavyo serikali yetu iko makini kuhakikisha vitendo vya rushwa vinazuiwa kwa sababu rushwa inauza haki hivyo basi unapopokea rushwa katika eneo la kazi anauza utu na usalama wa wafanya kazi,pia tumewafundisha weledi wa kutambua vihatarishi vya ajali katika maeneo ya kazi na jinsi gani waweze kutoa ushauri juu ya namna ya kuviondoa vihatarishi hivyo” amesema Khadija Mwenda, Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Aidha Bi. Khadija Mwenda aliongeza kuwa OSHA ipo zaidi kuhamasisha,kuelimisha na kushauri masuala ya usalama na afya kuliko kutoa adhabu maeneo ya kazi, pia amesisitiza kuwa OSHA ni taasisi rafiki ambayo nia na madhumini yake ni kuhamasisha na kukuza uwekezaji nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti, Takwimu na Uhamasishaji wa OSHA, Joshua Matiko amesema kuwa miongoni mwa sababu za kutoa mafunzo hayo ni kupata mrejesho wa changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika maeneo ya kazi na kuzipatia ufumbuzi.

“Baada ya mafunzo haya sisi tuna imani kuwa wakaguzi wote watakapo rudi katika maeneo yao ya kazi watafanya kazi kwa kuzingatia weledi na miiko ya utumishi wa umma na tunafikiria kuwa tunakutana kila mwaka ili kama kuna matatizo, maboresho na hata mafanikio watuambie kwasababu hatuwezi kuboresha huduma zetu pasipo kusikia mrejesho kutoka kwao” amesema Joshua Matiko.

Washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru OSHA kwa kuandaa mafunzo hayo huku wakikiri kuwa yamewaongezea hamasa ya kuanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia miiko ya maadili ya kazi.

“Mafunzo haya ya siku tano yameniongezea weledi mkubwa sana katika utendaji wangu mfano nimepata mafunzo ya kubaini vihatarishi katika maeneo ya kazi pamoja na mafunzo katika masuala yote yanayohusiana na ukaguzi hivyo kuwa ufupi mafunzo haya yataifanya OSHA kuboresha huduma zake katika maeno mbalimbali nchini.” Amesema Richard Edward, Mkaguzi wa Mazingira ya kazi.

Kwa upande wake Deborah Dickson amabye ni mkaguzi wa mitambo kutoka Ofisi za OSHA nyanda za juu kusini Mbeya amesema kuwa.mafunzo haya yataenda kuboresha utendaji kazi wao.

“Mafunzo haya yamegusa fani zote za washiriki mfano kuna wakaguzi wa umeme, mazingira, mitambo na wakaguzi wa afya, tunafanya kazi kila siku lakini kupitia mafunzo haya tumekumbushana miiko mbalimbali ya kazi na tutakapo rudi katika maeneo yetu ya kazi hatutafanya kazi kwa mazoea tena” alisema Debora.

OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Bunge,Uratibu,kazi,Vijana,Ajira na Wenye ulemavu yenye dhamana ya kusimamia utekelezaji wa Sheria na 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: