Mwenyekiti wa Chama cha WaganiTanzania (TSAEE), Profesa. Catherine Msuya akizungumza na maafisa Ugani waliohudhuria kwenye mkutano wa mwaka wa Chama hicho alipokuwa akifunga mkutano huo kwenye ukumbi wa Vijana, jijini Dodoma juzi.
Mkurugenzi Msaidizi wa utafiti, mafunzo na Ugani, Dkt. Kejeli Gillah (katikati) akizungumza na baadhi ya Maafisa Ugani waliohudhuria kwenye Mkutano wa Chama cha Wagani Tanzania (TSAEE) mara baada ya kumaliza mkutano kwenye ukumbi wa Vijana, jijini Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti, mafunzo na Ugani Dkt. Kejeli Gillah ( wa kwanza kulia) akibadilishana mawazo  na Mwenyekiti wa Chama cha Wagani Tanzania Prof. Catherine Msuya (kushoto) pamoja na wajumbe wengine mara baada ya kumaliza mkutano huo.
Mmoja wa washiriki wa mkutano wa Chama cha Wagani Tanzania (TSAEE) akichangia mada kwenye mkutano huo.
 


Na Mbaraka Kambona, Dodoma


MAAFISA Ugani nchini wametakiwa  kubuni mbinu na mifumo mbalimbali itakayowawezesha kuwasiliana kwa karibu na Watafiti, Wakulima, Wafugaji na Wavuvi ili waweze kuzalisha kwa tija hususan katika kipindi hiki ambapo Dunia inakabiliwa na  mabadiliko ya tabia nchi na maradhi ya corona.

Wito huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Wagani Tanzania (TSAEE), Prof. Catherine Msuya wakati akifunga mkutano wa mwaka wa chama hicho juzi jijini Dodoma.

Alisema kwa sasa kuna mabadiliko ya tabia nchi na maradhi ya korona hivyo lazima waendelee kujikita katika kubuni mifumo na teknolojia zitakazowasaidia kuwawezesha wananchi kuendelea kuzalisha kwa tija na kukabiliana na changamoto hizo.

" Najua tuna mashamba darasa lakini tuangalie mifumo mingine ambayo itaweza kutukutanisha wadau wote kwa pamoja kwa urahisi ili kuwasaidia wananchi wetu kwa lengo la  kuboresha mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi," alisema Prof. Msuya.

Naye, Afisa Kilimo kutoka Ilemela, Mwanza, Neema Semwaiko alisema kuwa kupitia mkutano huo wamejifunza mambo mbalimbali mazuri ikiwemo matumizi ya tehama katika kilimo ambazo watakwenda kuzitumia katika maeneo yao ya kazi kwa lengo la kuwawezesha Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kuzalisha kwa tija.

"Teknolojia hizi tulizopata tunajipanga kwenda kuzitumia kule tulipotoka kwa ajili ya kwenda kuboresha mawasiliano kati yetu sisi Wagani na Wakulima wetu na itatusaidia kuwasiliana na wadau wengi kwa wakati mmoja," alisema.

 Afisa Ugani kutoka Wilaya ya Mkuranga, Julitha Bulali  aliiomba Serikali kuendelea kuwawezesha Wataalamu wa ugani wa ngazi zote ili waweze kuwahudumia ipasavyo wananchi katika maeneo wanayofanyia kazi.

"Mkutano huu umetuwezesha kukutana sisi Maafisa Ugani kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na tumejifunza na kubadilishana uzoefu ambao utatusaidia kuboresha utendaji wa kazi zetu," alisema Bulali.

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: