Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela amewataka wadau wa sekta ya maji kujikita katika kutafuta miradi mikubwa itakayowasaidia kuepukana na changamoto za uhaba wa maji kwenye Wilaya za Mkoa wa Arusha na kuweza kutatua changamoto hizo.


Akifungua kikao kazi cha wadau wa sekta ya maji Mkoa wa Arusha, kilicholenga kujadili hali ya upatikanaji wa Maji nao utatuzi wa changamoto zake kinachofanyika Jijini Arusha,Mongela amesema changamoto ya uchache wa  maji katika wilaya zimekuwa zikisababisha migogoro katika jamii hususani wilaya ya Monduli katika baadhi ya maeneo.


Aidha Mongela amewataka viongozi wa Wilaya katika Mkoa wa Arusha,wenyeviti na wakurugenzi wa Halmashauri  pamoja na  watendaji wote kusimamia miradi ya maji ili ikamilike kwa wakati na katika muda uliopangwa ambapo amesema ili miradi hiyo iweze kukamilika inaitaji ushirikiano wa ngazi zote na wananchi kuweza kupata maji kwa wakati.


"Upungufu wa maji unapelekea huduma za afya na elimu kutokwenda vizuri kutokana na watumishi pamoja na wanafunzi kutafuta maji wakati wa kutoa huduma ikiwa wanafunzi kushindwa kusoma vizuri kwa ajili ya kutafuta maji, ni vyema mkafuatilia miradi hii ili wananchi waweze kupata maji safi na salama"alisema Mongella.


Vilevile Mongela amesena dhima ya Serikali ni kuhakikisha asilimia 85 ya wananchi vijijini wanapata maji safi na salama ,na asilimia 95 ya wananchi mijini wanapata maji safi na salama ifikapo mwaka 2025 ambapo lengo la ajenda za maji ni kupewa kipaumbele kutokana na mazingira yalivyo.


Naye Meneja wa watoa huduma za maji  RUWASA Makao Makuu,Valentina  Masanja kutokana na malalamiko ya watumishi juu ya changamoto hizo amesema bodi ya RUWASA imeshaongeza idadi ya watumishi watakao changia kuongeza kasi ya usambazaji wa miundominu ya maji ikiwemo mabomba na ufikishwaji wa fedha za utekelezaji wa miradi kwa wakati ili kuondokana na changamoto inayowakabili kwa sasa.


"Ni kweli kuna changamoto ya mabomba na changamoto hiyo haipo Arusha tu ipo nchi nzima na bado tuna changamoto ya watumishi hasa katika eneo la manunuzi ndio maana wakaomba mabomba yananunuliwe kwa pamoja kupitia mfumo maalum wa PV4R kwa sababu  maofisa manunuzi hao wapo makao makuu."Alisema Meneja huyo


Awali akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya,Mkuu wa Wilaya ya Monduli Frank Mwaisumbe alishari Mamlaka hiyo kuongeza uzalishaji wa maji katika vyanzo vikubwa kwa vijijini kutokana na vyanzo vilivyopo sasa kuwa ni vyanzo vidogodogo ambapo huchangia migogoro katika vijijini hususani kwenye wilaya za wafugaji.


"Bado kuna kazi kubwa inatakiwa kufanyika ukizingatia wilaya nyingi zilizopo katika Mkoa wa Arusha maji hayakidhi mahitaji ya watu hususani wilaya zilizo kwenye ukame na vyanzo vichache vya maji na kwa sababu hiyo hupelekea wakazi wengi kukosa maji ikiwa wengi wao wapo katika maeneo yenye miundombinu hafifu ya maji."Frank Mwaisumbe Mkuu wa Wilaya ya Monduli


Vilevile Mwaisumbe alisema Wilaya ya Monduli ina asilimia 71 ya upatikanaji wa maji na kwa uhalisia takwimu hizo haziendani na hali halisi ya upatikanaji wa maji wa sasa na haziendani na kasi ya Serikali ya awamu ya sita katika uwekezaji wa viwanda.


"Hatuwezi kuzungumzia viwanda kama hatuna maji,katika maeneo mengi kuna vyanzo vikubwa hivyo tunawaomba wadau pamoja na ofisi ya Mkuu wa Mkoa kubuni miradi mikubwa ambayo inaweza kuleta tija na kuwafikia watu wengi zaidi ili kuongeza maendeleo ya kiuchumi na kijamii,"alisema Mwaisumbe.


Mwaisumbe amesema miradi mikubwa ya Maji ndio itatatua changamoto ya Maji kwa kiasi kikubwa hasa kwa Jamii za wafugaji kuliko miradi midogo inayowafikia wananchi wachache.


Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki Mhe.John Danielson Palangyo katika kikao kazi hicho ameipongeza RUWASA kwa kufanya kazi vizuri pamoja na kuwa ni taasisi changa,bado wameonysha kufanya kazi kwa juhudi na kujituma.


Ameongeza kuwa kupitia fedha za UVIKO 19 zilizotolewa zinapaswa kutumika vizuri ili kuweza kukamilisha miradi wakati kwani muda uliotolewa wa matumizi ni mchache sana.


"Mhe.Rais alisema fedha hizo muda wake ni miezi 9,kwa hiyo ni lazima RUWASA wajipange sawasawa vinginevyo wanaweza wakaleta maneno kwani Meru kuna vijiji ambavyo havijapata maji ukilinganisha na miradi tuliyonayo ya mwaka huu ni bilioni 2.4,kifupi kuna miradi ambayo fedha zake zimetengwa kwenye bajeti lakini hazijatolewa hivyo kuchelewesha utekelezani wa miradi."Alisema Mhe.Mbunge

Share To:

Post A Comment: