Na WAMJW - Katavi
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameitaka
Wizara ya Afya kurejesha usimamizi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Katavi kwa Katibu Tawala Mkoa wa Katavi.
Mhe. Kassim
Majaliwa amesema hayo mara baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi
wa jengo la Hospitali hiyo Katika Manispaa ya Mpanda na kuonyesha
kutoridhishwa na kasi ya ujenzi.
“Moja ya malengo ya ziara yangu
ni kuja kuona ujenzi wa jengo hili, ujenzi wa jengo hili umesuasua sana,
haujaniridhisha” amesema Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa
Mhe.
Kassim Majaliwa amesema kuwa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Katavi umeanza toka mwaka 2018 huku hadi kufikia mwezi huu hatua za
ujenzi zimefikia asilimia 45 na kuleta sintofahamu kwa wananchi katika
uhakika wa upatikanaji wa huduma bora za matibabu ya rufaa jirani na
makazi yao.
Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Kassim Majaliwa amemuagiza
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel kurejesha haraka usimamizi wa
ujenzi wa Hospitali hiyo kwa Katibu Tawala Mkoa wa Katavi ili wawe
wasimamizi wakuu na karibu katika mradi huo.
“Kama Mikoa mingine
tumetumia Makatibu Tawala kujenga, nyie mlimpa Katibu Tawala Mkoa
kujenga, mkarudisha Wizarani ambapo wataalam mpo Dodoma, jengo liko
Katavi, mtaweza kweli kusimamia ujenzi?” amehoji Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia
Suluhu Hassan imejipanga kusogeza karibu huduma za matibabu kwa wananchi
na tayari Mheshimiwa Rais ametoa kiasi cha Shilingi Milioni 688 kwa
ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali hiyo.
Mhe. Kassim
amemuagiza Katibu Tawala Mkoa wa Katavi kuunda kamati ya usimamizi wa
ujenzi wa Hospitali hiyo na kuitambulisha kwa viongozi ndani ya Mkoa huo
ili nao waweze kusimamia kwa ukaribu hatua za ujenzi wa Hosptali hiyo
huku akiwaonya kutumia vyema fedha hizo ili kuweza kukamilisha upande
mmoja wa jengo hilo ili huduma zianze kutolewa kwa wananchi.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa
maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Wizara
imeyapokea na kuanza utekelezaji wa mara moja kuhakikisha fedha
zilizotolewa zinasimamiwa na Katibu Tawala Mkoa wa Katavi.
Dkt.
Mollel amesema kuwa kwa kipindi kilichobaki cha miezi 10 Wizara
itahakikisha inashirikiana kwa ukaribu zaidi na Uongozi wa Mkoa wa
Katavi ili kuweza kukamilisha lengo kusudiwa na huduma za matibabu
zianze kutolewa kwa wananchi.
Awali akisoma taarifa ya mradi wa
ujenzi wa hospitali hiyo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tiba Dkt.
Caroline Mayengo amesema kuwa ujenzi wa Hospitali hiyo unatarajia
kugharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 12.2 chini ya uratibu wa Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mkandarasi
SUMA JKT na Mshauri Elekezi Crystal Consultants.
Dkt. Caroline
amesema kuwa ujenzi wa Hospitali hiyo unatekelezwa kwa awamu kulingana
na upatikanaji wa fedha. Awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huu ilianza
na majengo mawili ambayo ni jengo kuu lenye ghorofa moja lenye Kitalu A
na B litakalotoa huduma za afya ya uzazi mama na mtoto (Maternity),
huduma za dharura (EMD), wagonjwa wa Nje (OPD), Famasi, huduma za
Radiolojia, Huduma za upasuaji na huduma za uangalizi Maalumu (ICU)
pamoja na jengo la Maabara.
Post A Comment: