Timu ya Viongozi wa Taasisi ya Elimu ya Watu wazima nchini (TEWW) mkoani Iringa wakiwa wamemtembelea mmoja wa wasichana aliyekatisha masomo yake baada ya kupata ujauzito ili arejee shuleni.
Mmoja wa Mabinti (katikati) ambaye ndoto zake zilizima baada ya kupata ujauzito akiwaelekeza wenzake baada ya kurudi shule kupitia mpango wa TEWW.
Baadhi ya walimu na wanafunzi wanaosoma kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu wazima nchini (TEWW) mkoani Iringa kupitia Kituo cha Sabasaba wakiwa katika picha ya pamoja.


Na Mwandishi wetu, Iringa


TAASISIi ya Elimu ya Watu wazima nchini (TEWW) inatekeleza mpango wa kuwasaidia wasichana waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwamo mimba, kumaliza elimu ya sekondari.

Taasisi hiyo imebeba jukumu la kuwasaidia wasichana hao wakati ambapo  bado sera ya elimu ikiwa haijaruhusu, kuendelea na masomo kupitia mfumo wa kawaida.

Mkurugenzi Mkuu wa TEWW, Dkt Michael Ng’umbi amesema katika taarifa yake kuwa kwa namna ya pekee mfumo huo umekuwa mkombozi kwa wasichana waliopata changamoto na kulazimika kuacha masomo yao.

“Kuna ushuhuda wa wasichana ambao wamefanya vizuri sana katika masomo yao kwa kupitia vituo vya elimu kwa njia mbadala vinavyosimamiwa na TEWW,” amesema Dk Ng’umbi.

Akitoa mifano, amesema katika mwaka 2020, wasichana kumi kutoka mkoa wa Tanga waliosoma kupitia mfumo huo walifaulu vizuri na kujiunga na vyuo vya elimu ya juu.

“Wasichana hawa ni miongoni mwa wasichana waliosoma katika vituo vinavyosimamiwa na taasisi hii, kupitia ufadhili wa shirika la BRAC Maendeleo,” anasema Dk Ng’umbi.

Alisema katika mkoa huo wa Tanga,  mwaka 2020 wasichana 31 walifaulu mtihani wa kidato cha nne kati ya daraja la kwanza na la tatu. 

“Kati yao, 20 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika shule za serikali na sita  kujiunga na vyuo vya serikali,” alisisitiza.

Akielezea mkoa wa Mwanza, Dk Ng’umbi alisema mwaka 2019, wasichana 37 walifaulu mtihani wa kidato cha nne daraja la kwanza hadi la tatu na kuwa kati yao, tisa walichaguliwa kuendelea kidato cha tano na 12 walijiunga na vyuo. 

Aidha katika mwaka 2020, wasichana 24 wa mkoa wa Mwanza walifaulu mtihani huo kwa daraja la 1 hadi la 3, kati yao 11 wamechaguliwa kuingia kidato cha tano na 12 wanaendelea na mafunzo vyuoni. 

Mwaka 2020 mikoa ya Kigoma na Dodoma kila mmoja ulipata msichana aliyefaulu kiwango cha daraja la kwanza.

Baadhi ya wasichana waliosoma kupitia mfumo huo waliishukuru taasisi hiyo kuwa daraja kwao na kuhakikisha wanatimiza ndoto zao.

Mmoja wa wasichana hao, ambaye anasoma kituo cha sabasaba alisema, ndoto zake zilikufa alipoacha masomo yake kwa sababu ya mimba lakini sasa anauhakika.

Kwa upande wake, Mkufunzi Mkazi wa Mkoa wa Iringa, Camilius Mwila amesema Iringa ni kati ya mikoa inayotekeleza kwa vitendo, elimu hiyo.

Taasisi hiyo ilianza kuendesha masomo ya sekondari kwa njia mbadala mwanzoni mwa miaka ya 1970. 

Share To:

Post A Comment: