Wizara ya kilimo  imebainisha kuweka mikakati ya  kukabiliana na sumu kuvu kwa kuanza ujenzi wa miundo mbinu sahihi ya kuhifadhia mazao na   kutoa elimu shirikishi kwa wakulima  na wasindikaji  kwa lengo la kukabiliana na sumu kuvu Nchini


Hayo yamebainishwa leo jijini hapa na  Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usalama wa chakula Bi.Josephine Amollo wakati akifungua semina  ya waandishi wa habari 100 kutoka mikoa 9  hapa nchini juu ya uchafuzi wa sumu kuvu na athari zake katika usalama wa chakula afya na uchumi.


Amesema tatizo la sumu kuvu sio Tanzania tu bali ni tatizo la nchi nyingi na mara nyingi husababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi lakini serikali imejipanga kuhakikisha kuwa kinachozalishwa kinakuwa salama.


"Nchi yetu iko salama na chakula kipo salama hakuna tatizo kama ilivyokuwa mwaka 2016 baada ya watu kudhurika na masuala ya sumu kuvu.


" Lengo la kuwapa elimu hii waandishi wa habari tunataka wakawe walimu wakaielimishe jamii na kuondoa taharuki ambayo inaleta sintofahamu kwa jamii tunaamini wanahabari hawa watafikisha elimu sahihi kupitia vyombo vyao vya habari,"alieleza.


Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa mazao ambayo yanaathirika zaidi na sumu kuvu ni mahindi na Karanga na kuitaka jamii kufuata utaratibu sahihi kuanzia wakati wa kupanda hadi kuhifahi mazao yao.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Kilimo Revocatus Kasimba amesema toka mradi huu wa kudhibiti sumu kuvu kuanzishwa kumesaidia kupunguza kuenea kwa janga hili na kupelekea wakulima kuzalisha mazao yenye tija.


Amesema ili kudhibiti kuendelea kutokea kwa sumukuvu ni vyema mikakati madhubuti ikawekwa ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wakulima na watumiaji wa mazao ya chakula kama Karanga na Mahindi.


"Naomba waandishi wa habari mtumie vizuri semina hii ya siku mbili kwasababu jamii inawategemea, ukitumia hata kipande cha sekunde 10 kutoa elimu kuhusu sumukuvu utakuwa umeokoa kizazi cha sasa na badae," amesema 


Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma(CPC) Mussa Yusuph aliipongeza wizara ya kilimo  kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo  kwa waandishi wa habari kwani wengi wamekuwa wakiripoti lakini sio kwa upana.


Amesema mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uelewa kwa waandishi na kutoa taarifa ambazo zimekamilika na hatimae kupitia wao jamii itaelimika na kubadilika.


"Naipongeza Wizara ya kilimo na serikali kwa ujumla kwa kufanikisha mafunzo hayo kwa waandishi wa habari ambapo baada ya kumalizika yatazaa matunda kwa jamii kupitia vyombo  vya habari wanaripoti" alisema Mussa Yusuph.


Semina hii ya waandishi wa habari 100 kutoka mikoa 9  hapa nchini juu ya uchafuzi wa sumu kuvu na athari zake katika usalama wa chakula afya na uchumi imeanza leo Tarehe 18 na itamalizika Tarehe 19 mwezi huu 2021.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: