Msajili wa Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB), Mhandisi Patrick Barozi, akizungumza na wahandisi walioshiriki mafunzo ya ukaguzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), kipande cha Morogoro hadi Makutupora (Km 422) kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo utekelezaji wa mradi huo.

Meneja Msaidizi wa mradi wa Reli ya Kisasa kipande cha Morogoro hadi Makutupora (Km 422) kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Christopher Mang’wela, akitoa elimu kwa Wahandisi waliotembelea mradi huo ili kujifunza kwa vitendo utekelezaji wake, jijini Dodoma. Mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 61.

Mkurugenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa, Mhandisi Faustine Kataraia, akijibu baadhi ya maswali yalioyoulizwa na wahandisi (hawapo pichani) waliotembelea mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa kipande cha Morogoro hadi Makutupora (Km 422), jijini Dodoma.

Kazi za ujenzi wa Reli ya Kisasa kipande cha Morogoro – Makutupora (Km 422) zikiendelea jijini Dodoma. Ujenzi wa kipande hicho umefikia asilimia 61.

Wahandisi kutoka Serikalini na Sekta Binafsi wakioneshwa kwa vitendo namna ya uwekeaji wa mataruma katika ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha Morogoro – Makutupora (Km 422), jijini Dodoma.

Wahandisi kutoka Serikalini na Sekta Binafsi wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kutembelea na kujionea vitendo namna ya uwekeaji wa mataruma katika ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha Morogoro – Makutupora (Km 422), jijini Dodoma.


Imeelezwa kuwa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), unatarajiwa kuwekwa mifumo ya kisasa ambayo itasaidia kuzuia ajali ambazo zinaweza kujitokeza wakati wa uendeshaji wa reli hiyo na ambao hautamruhusu dereva kuzidi ama kupunguza mwendo uliowekwa.

Hayo yamesemwa na Meneja Msaidizi wa mradi wa reli ya Kisasa, kipande cha Morogoro - Makutopora (Km 422) kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Christopher Mang’wela, wakati akizungumza na wahandisi kutoka Serikalini na Sekta Binafsi ambao wametembelea mradi huo uliofika asilimia 61, jijini Dodoma, kwa ajili ya kujifunza utekelezaji wa mradi kuanzia hatua mbalimbali zilizotekelezwa.

“Kama mnavyoona, mradi umefika asilimia 61, na uendeshaji wake utakuwa ni wa kisasa kwani utawekwa vifaa maalum vya kumuongoza dereva wa treni ili kuzuia ajali.” amesema Mhandisi Mang'wela.

Awali, akizungumza kwa niaba ya wahandisi hao, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Mhandisi Patrick Barozi, ameeleza kuwa anaona nia ipo na uwezo kwa watanzania katika kusimamia miradi mikubwa inayoendelea nchini huku tukiwa na usimamizi mdogo kutoka wenzetu wa nje na hivyo kuwaleta wahandisi wetu katika mradi kutaongeza chachu ya kuchukua zabuni nyingi za miradi mikubwa inayoatarajiwa kuanza na kuendelea hapa nchini.

"Tumetembelea mradi huu katika baadhi ya maeneo ambapo tumeridhishwa na mradi huu na tumeona unaendeshwa vizuri kuanzia mwanzoni hadi hapa ulipofika kwani kupitia mradi huu wahandisi wamejifunza mengi", amefafanua Mhandisi Barozi.

Aidha, Mhandisi Barozi ameongeza kuwa kupitia vipande vitatu vya utekelezaji wa mradi huo, wahandisi wa hapa nchini wamepata utaaalamu wa kutosha na hivyo kuweza kuisaidia Serikali kwa utekelezaji wa awamu zinazofuata endapo watawezeshwa katika suala zima la upatikanaji wa vifaa.

Kwa upande wake, Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mhandisi, Dkt. Ramadhan Mlinga, amesema kuwa wahandisi waliopo kwenye mradi huo kufuatilia kwa makini kipindi cha mwisho cha utekelezaji wa mradi huo kwani kipindi hiki husaidia kuboresha utekelezaji wa miradi inayofuata kwa kuangalia changamoto zilizowakabili katika utekelezaji wa mradi uliopita na kutafutia ufumbuzi katika utekelezaji wa mradi ujao.

"Kwa kawaida miradi ina hatua tano za utekelezaji ikiwemo kuibua mradi, kupanga jinsi ya kutekeleza mradi, utekelezaji wa mradi, ufuatiliaji wa utekelezaji wa mradi na kufunga mradi ambapo hivi ni lazima vizingatiwe ili mradi ufanikiwe”, amesisitiza Mlinga

Naye, Mhandisi kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Nyandalo Hezron, amesema kuwa wamefurahishwa na mafunzo hayo kwani yamewasaidia kujua uhalisia wa yale waliyojifunza darasani na kuyaleta katika utekelezaji ambayo yawakumbusha miongozo mbalimbali katika usimiamizi wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi inayoendelea.

Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) ulioanza mwezi Aprili 2017 wenye lengo la kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji nchini na nchi za jirani unaendelea kutekelezwa ambapo hivi karibuni kazi za ujenzi sehemu ya Isaka – Mwanza yenye urefu wa kilometa 341unatarajiwa kuanza.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: