Na Asteria Muhozya, Njombe

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amemwagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe kufanya ukaguzi wa Leseni zote 245 za Uchimbaji Madini mkoani humo ili kujua maendeleo ya uendelezwaji wake.

 

Agizo hilo linafuatia ombi lililowasilishwa na wachimbaji wadogo wa Madini mkoa wa Njombe ambao wameiomba Wizara kuwapatia maeneo ya kuchimba kutokana na sehemu kubwa kushikiliwa na wawekezaji kwa kipindi kirefu pasipo kuyaendeleza.

 

 "Nakuagiza RMO fanya uchambuzi wa Leseni zote kujua zina hali gani, ikiwa zinalipiwa, ni maendeleo gani  yamefanyika ili kuanzia hapo wizara ichukue hatua. Tunapotoa leseni tunataka watu waziendeleze na wachimbe siyo kuzifungia kabatini,’’amesisitiza Prof. Msanjila.

 

Prof. Msanjila ameongeza kuwa, moja ya vipaumbele vya Serikali na kama alivyoeleza Waziri wa Madini katika Hotuba yake ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 ni pamoja na kuwaendeleza, kuwarasimisha na kuwapatia maeneo wachimbaji wadogo   ili wachimbe, hivyo, wizara itahakikisha inalifanyia kazi kwa karibu suala hilo.

 

Amefanunua kuwa, endapo mmliki wa leseni ana nia ya kuiuza leseni yake hakatazwi isipokuwa anapaswa kuiendeleza kwanza kabla ya kufanya maamuzi mengine. ‘’ Ukitaka kuuza leseni lazima useme uliifanyia nini kabla ya kuiuza. Huu ndiyo utaratibu wa Sheria,’’ amesema.

 

Akizungumzia mwenendo wa makusanyo katika mkoa huo amesema bado kiwango kiko chini ikilinganishwa na rasilimali madini zinazopatikana katika mkoa huo ikiwemo chuma na makaa ya mawe na kuongeza kwamba, hadi sasa Mkoa wa Njombe umekusanya kiasi cha shilingi milioni 240 kati ya shilingi bilioni 1 uliyopangiwa kukusanya huku akitaja moja ya sababu ikiwa ni wamiliki kutozifanyia kazi leseni zao.

 

Pia, ametumia fursa hiyo kuwapongeza wachimbaji wadogo katika mkoa huo kwa kufanya shughuli zao huku wakishirikiana kwa karibu na Ofisi ya Madini pamoja na ofisi ya Mkoa wa Njombe suala ambalo limepelekea kutokuwepo kwa migogoro inayozuia maendeleo ya Sekta.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Njombe Alfred Luvanda, amemhakikishia Prof. Msanjila kuwa, wachimbaji mkoani humo wako tayari kimitaji ikiwemo kulipa kodi za serikali pindi itakapowapatia leseni za kuchimba madini, huku wakiahidi kuendeleza ushirikiano na Ofisi ya Madini.

 

‘’Kwanza tunashukuru sana kwa ujio wako, tunaamini kilio chetu kimefika sehemu sahihi.  Tunakuahidi tutachimba, tutalipa kodi za serikali na tutaipa serikali heshima,’’ amesema Luvanda.

 

Naye, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Njombe Henry Mditi amewaeleza wachimbaji hao kuwa ofisi ya madini mkoani humo haitomuonea mtu yoyote na hivyo akawataka wachimbaji hao kufanya shughuli zao kwa kufuata Sheria.

 

Prof. Msanjila amekutana na wachimbaji hao Mei 13, 2021, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo iliyolenga kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wachimbaji pamoja na watumishi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

 

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: