OFISA anayshughulikia malalamiko wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Makwinja Dismas Yusuph akizungumza wakati wa mafunzo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga
Watendaji wa TASAF kutoka Halamshauri 35 waliohudhuria mafunzo hayo ya siku mbili wakifuatilia matukio mbalimbali


Na Mashaka Mhando,  Tanga
 
MATUMIZI ya mfumo wa kuweka kumbukumbu, utasaidia kupunguza malalamiko ya wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia mradi unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji wa TASAF kutoka halmashauri 35 za mikoa ya Tanga, Morogoro, Kilimanjaro, Arusha na Pemba, Ofisa anayeshughulikia malalamiko wa mfuko huo, Makwinja Dismas Yusuph alisema mfumo huo utapunguza malalamiko kwa kiasi kikubwa. 

"Madhumuni ya mafunzo haya kwa watendaji wetu kutoka halmashauri za wilaya na majiji 35, utasaidia kupunguza malalamiko ambayo mara nyingi yamekuwa yakitolewa na walengwa wa mpango wa kunusuru kaya masikini," alisema Makwinja. 

Alisema mpango wa kunusuru kaya masikini wamekuwa wakitoa ruzuku kwa kaya zinazostahili kwa kukidhi vigezo vya elimu, afya na lishe. 

"Sasa unapokuwa na mradi kama huu (Social Protection)  lazima unazalisha malalamiko mengi kwasababu unagusa jamii moja kwa moja na malalamiko ni mengi, " alisema. 

Ofisa huyo alisema kufuatia hali hiyo mpango umeweka kitengo maalum (Call Center) chenye wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali utakaoshughulikia malalamiko yatakayotolewa. 

Alisema kitengo hicho kitapokea simu za malalamiko, itayachunguza kama yana ukweli kisha watayapatia ufumbuzi tofauti na utaratibu wa zamani wa kupokea taarifa zilizoandikwa kwenye makaratasi. 

Makwinja alibainisha miongoni mwa malalamiko yanayotolewa mara kwa mara na wanufaika hao, ni pamoja na kukatwa fedha zilizotokana na wao kushindwa kukidhi vigezo vilivyowekwa na mfuko. 

"Hapa ni lazina niseme kwamba sababu kubwa ni elimu kwa wanufaika maana wakati mwingine wanakiuka taratibu tulizoziweka hasa katika suala la elimu, afya na lishe, " alisema Makwinja na kuongeza, 

"TASAF haigawi fedha tu kama wengi wanavyodhani, tunahaulisha kwa kutoa ruzuku kiasi kidogo cha fedha ili kuleta matokeo katika kaya masikini kwa kiwango kidogo wanachopewa, " 

Alisema fedha hizo wanataka zilete tija kwa wanafamilia kwa watoto kwenda shuleni na kuhudhuria masomo kwa kiwango cha walau asilimia 80, kupata huduma za afya pamoja na lishe bora. 

Hata hivyo, ofisa huyo aliwataka watendaji waliopatiwa mafunzo hayo waone wajibu wa kile walichojifunza wakakitekeleze kwa kutumia ujuzi utakaosaidia mradi huo kuwa na kumbukumbu sahihi zitakazohifadhiwa kwa njia ya eletroniki. 

Hadi sasa mfuko wa Tasaf umeweza kuhudumia Kaya masikini zipatazo milioni moja na laki moja nchini kupitia mpango huo (SDGs). 
 
MWISHO


Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: