Na,Jusline Marco;Arusha

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Dkt.Avemaria Semakafu amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Meru Emmanuel Mkongo kuweka utaratibu wa utipaki wa takataka kwa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao pembezoni mwa uzio wa shule ya sekondari elimu maalum Patandi ili kuyaweka mazigira ya shule hiyo katika hali ya usafi.

Dkt.Semakafu ameyasema hayo katika ziara ya ukaguzi wa shule hiyo iliyoifanya leo ambapo amebainisha changamoto hiyo kutokana na wafanyabiashara hao kugeuza eneo la shule kama sehemu ya dampo hali ambayo itahatarisha afya za wanafunzi pindi watakaporipoti shuleni hapo.

"Sisi kwetu shule ni mahali salama na hawa ni watoto wenye mahitaji maalum kwani zimetimika fedha nyingi katika kujenga shule hii,sasa hatukuijenga hii shule ili egeuke kuwa jalajala hivyo shule hii haitafunguliwa hadi pale mazingira yake yatakapo kuwa safi."alisema Dkt.Semakafu

Aidha Dkt.Semakafu ametoa muda wa wiki moja kwa mwenyekiti wa kamati ya ujenzi ambaye pia ni mkuu wa chuo cha ualimu elimu maalum Patandi,Lusian Segesela kuhakikisha wanapokea vifaa vyenye ubora unaostahili ikiwa ni pamoja na kuondoa samani ambazo hazijakidhi vigezo vinavyojitajika.

Vilevile ametoa wiki moja kwa mkuu huyo kuhakikisha walimu wanaosomea ufundishaji wa wanafunzi wa elimu maalum kufanya usafi katika eneo hilo la shule sambamba na upandaji wa miti na bustani mbalimbali ili kuyaweka mazingira katika hali inayovitia.

"Katika moja ya vipindi vyao wahakikishe hili eneo lote la shule ya sekondari elimu maalum limekaa kama mahali salama na rafiki kwa mtoto mwenye uhitaji maalum kwahiyo wanafunzi wote wagawiwe maeneo ya kufanya usafi iwe ni eneo lao la kazi za mikono."Alisisitiza Dkt.Semakafu

Pamoja na hayo amesema kuwa lengo la wizara ya elimu,sayansi na teknolojia ni kuwa na shule maalum moja kila Mkoa
wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari ya elimu maalum kufanya marekebisho ya vifaa vyote visivyokuwa na ubora pamoja na kuhakikisha vifaa wanavyovipokea kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo vinakuwa na ubora unaostahili.

Ameongeza kuwa ujenzi wa shule hiyo ni muitikio wa agizo la serikali ya awamu ya tano ya kuhakikisha fursa za elimu kwa wanafunzi wote zinatolewa kwa kutatua changamoto ambazo watoto wenye uhitaji maalum wanazipata kwa kuanzisha mradi huo wa ujenzi wa shule maalum ambapo mpaka sasa shilingi bilioni 3.4 zimeweza kutumika katika ujenzi huo ikiwa ni awamau ya kwanza upande wa shule ya sekondari.

Kwa upande wake Mhandisi mshauri katika mradi huo Injinia Saidi Shaushi ameahidi kuzishughulikia changamoto ambazo zimeonekana katika ukaguzi huo na kuzimaliza kwa wakati ndani ya muda walipewa na Naibu Katibu mkuu wa wizara ya elimu,sayansi na teknolojia Dkt.Avemaria Semakafu.

Naye mwenyekiti wa ujenzi huo ambaye pia ni Mkuu wa chuo cha ualimu elimu maalum Patandi Wilayani Arumeru Lusian Segesela amesema kuwa pamoja na shughuli za utekelezaji za chuo pia walikabidhiwa jukumu la kusimamia ujenzi wa shule hiyo kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum ambapo ujenzi huo umefikia asilimia zaidi ya 95 ili uweze kukamilika.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: