Mkuu wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila amewataka wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa masomo 2019/20  kuhakikisha wanazingatia kile kilichowapeleka chuoni hapo kuwa ni kusoma na kufanya vizuri katika mitihani yao na si vinginevyo.

Prof. Mwakalila ametoa kauli hiyo leo wakati alizungumza na wanafunzi wanaosomea cheti, dipoloma na wale wa digrii ambapo kwa ujumla amewataka wanafunzi hao  kujiepusha  na vitendo vyote vinavyoashiria ubaguzi, masuala ya kisasa, kuhakikisha wanakuwa na nidhamu pamoja na kuwa na matumizi mazuri ya muda ili kufikia malengo wanayokusudia.

“ Lengo la kuzungumza na ninyi kwanza ni kuwapongeza kwa kuchaguliwa katika Chuo hiki kikongwe Cha Mwalimu Nyerere, ambacho kina historia kubwa na pia kimebeba jina Kubwa la Muasisi wa Taifa letu, kuhakikisha kile kilichowaleta hapa kitaaluma mnakifanikisha ikiwa ni pamoja na kusoma kwa bidii na Maarifa na kumtanguliza Mungu mbele, mambo ambayo hayana msingi achaneni nayo,”alisisitiza Prof. Mwakalila.

“Msipoteze malengo ambayo yamewaleta hapa, mmekuja kusoma zingatieni hilo na wala msijiingize kwenye mambo ambayo yatawapotezea muda, na mnapopata changamoto mbalimbali basi viongozi wa Chuo tupo na hata Serikali ya Wanafunzi ipo kwa ajili ya kusikiliza na kupatia ufumbuzi changamoto hizo”, aliongeza Prof. Mwakalila.

Mkuu huyo wa Chuo  amesema  Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kina historia iliyotukuka, kina jina kubwa, vijana wengi wanamsoma tu Baba wa Taifa kwenye vitabu lakini ni mtu muhimu sana kwa Taifa letu.

Amesema muasisi wa Chuo Cha Mwalimu Nyerere  ni Rais wa Kwanza wa Taifa hili ambaye ni hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo  mawazo  ya kujenga Chuo kwa ajili ya wazalendo yalianza mwaka 1958 ambapo Chuo kilifunguliwa rasmi Julai 29, 1961, hivyo Chuo hiki ni kikongwe.

Prof. Mwakalila aliongeza kuwa Lengo la Chuo wakati kinaanzishwa likiwa ni  kwa ajili ya  kuandaa viongozi wazalendo ambao lazima waandaliwe, ili kwenda kuongoza nchi, hivyo amewahakikishia wanafunzi kuwa wapo kwenye Chuo ambacho kitawajenga kimaadili na kizalendo kwa ajili ya kuwa viongozi wazuri wa baadae.

Imetolewa na;
Kitengo Cha Habari na Mawasiliano,
Chuo Cha KumbuKumbu ya Mwalimu Nyerere
8/11/2019
Share To:

msumbanews

Post A Comment: