NAIBU Waziri wa Nishati Subira Mgalu katikati akikata utepe kuashiria uzinduzi wa nishati ya umeme kwenye Kijiji cha Stesheni wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani kulia ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Juma
Naibu Waziri Nishati Mhe.Subira Mgalu amelitaka Shirika la Umeme Tanzania, (Tanesco) kujiendesha kibiashara ,Kiuchumi ikiwemo kihuduma zaidi kwa wananchi kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini
Naibu Waziri ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kalabaka , Kata ya Misugusugu katika wilaya ya Kibaha mjini,Mkoani Pwani ambapo alisema shirika hilo linatakiwa kuthamini wateja kwakuwa wateja ndio msingi mkuu wa kuendesha shirika, na hivyo ni jukumu la shirika kuhakikisha wateja wanahudumiwa kwa wakati hasa kuunganishwa na huduma ya umeme mara tu baada ya kulipia.
“Kama mteja amelipia pesa aliyotakiwa kulipa kwanini asiwekewe umeme, unamsubirisha miezi 3, yote ya nini, Hii inakua ni uonevu kwa wateja,mteja afungiwe umeme ndani ya muda mfupi kama ilivyoagizwa, alisema Naibu Waziri .
Sambamba na hilo Naibu Waziri pia aliwataka waataalamu wa TANESCO kuyaangalia maeneo ya barabarani , kwani ni maeneo ambayo yanauhitaji sana ya Umeme hasa kutokana na maeneo hayo kuwa maeneo ya biashara na hivyo wafanya biashara wengi wanahitaji umeme , hivyo hiyo ni fursa Nzuri ya kibiashara kwa TANESCO na wananchi kwa ujumla na kusema wananchi watakaolipia wapate huduma kwa haraka sana .
“Wateja watakaolipia mapema kwa kuwa wanauhitaji wa umeme haraka naomba wahudumiwe kama first track”alisema mhe.Mgalu
Akizungumzia hali ya usambazaji wa Umeme katika wilaya ya Kibaha, Naibu Waziri amesema kuwa Serikali imeamua kuwekeza Kibaha kwa kuwa ni eneo lenye mahitaji makubwa ya Umeme ikiwemo uwepo wa viwanda mbalimbali,
Alisema kwamba Serikali imetoa kiasi cha takribani Bilioni 17na Dola milioni 4 ili kusambaza umeme katika vijiji vya Pwani ikiwemo kibaha kupitia miradi mbalimbali ya Umeme pamoja na mradi wa Periurban ambao mpaka Sasa mkandarasi Sengerema ameshafikia asilimia 90 yautekelezaji,na kazi itakayobaki ni kuunganisha tu wateja.
Aidha amewataka wananchi ambao bado hawajafikiwa na huduma ya Umeme kuwa na Subira kwani Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanapata Umeme, na kuwataka wananchi kutambua kuwa serikali inatekeleza pia miradi mingine ya kimaendeleo kama vile ujenzi wa zahanati na hospitali, ujenzi wa madaraja, ujenzi wa barabara na Shule na miradi mingi yote ni kwaajili ya wananchi, hivyo wanapochelewa kupata Umeme wasilalamike badala yake wajue kuwa umeme utafika na huduma zingine pia zinatakiwa kuwafikia.
Naye Mbunge wa Kibaha vijijini Mhe.Hamood Juma ameishukuru Serikali kwa kufikisha Umeme kijiji cha Mpiji stesheni na kuipongeza TANESCO kwa kutoa ushirikiano mzuri kwa wananchi na uongozi wa Wilaya ya Kibaha vijijini katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya Umeme.
Naibu Waziri wa Nishati Mhe.Subira Mgalu ametembelea vijiji 6katika wilaya ya kibaha vijijini na mjini, ambapo amewasha umeme katika kijiji cha Mpiji stesheni na kukagua kazi ya kuunganisha umeme wilayani hapo ,kuongea na wananchi juu ya maoni yao juu ya masuala ya umeme , na kuwahakikishia kuwa huduma ya umeme itawafikia kwani umeme hautabagua nyumba Wala mtu, ni huduma kwa wote




Post A Comment: