Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amegawa kadi za CCM kwa wanachama kutoka Chadema katika Kijiji cha Narakauwo, Kata ya Loiborsiret wilayani Simanjiro.

Wananchi wanaodaiwa kuwa 3,500 ni wale ambao awali walikuwa CCM na kujiondoa na kujiunga na Chadema baada ya kukatwa majina ya baadhi ya wagombea waliokuwa wakiwaunga mkono katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Baada ya kurejea CCM jana, walisema wanaunga mkono utendaji wa Mnyeti na wa Rais John Magufuli.
Mnyeti, ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya siasa ya CCM Mkoa wa Manyara kabla ya kuwakabidhi kadi wanachama hao, katibu wa chama hicho wilayani Simanjiro, Ally Kidunda alimuomba afanye kazi hiyo.
“Kwa sababu wewe ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa naomba uje ufanye kazi hii ya kuwapokea na kuwakabidhi kadi za CCM miongoni mwa hawa wanachama wapya 3,500 waliorudi CCM,” alisema Kidunda.
Kidunda alisema Narakauwo hakuna upinzani ila wanachama hao waliondoka kwa hasira kuhamia upande wa pili lakini sasa wamerudi nyumbani.
Mmoja kati ya wanachama waliorejea CCM, Mathayo Lesenga alisema waliondoka baada ya wagombea waliokuwa wanawaunga mkono kukatwa majina yao.
Lesenga alisema wananchi wa eneo hilo walikuwa na imani na CCM lakini baada ya kuona kunafanyika ukiritimba walijitoa na kuhamia Chadema ila wamerudi ili kumuunga mkono Rais Magufuli na Mnyeti.
Mnyeti akizungumza na wananchi wa eneo hilo alitoa onyo kwa baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo akidai wanaandaa mgombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Alisema kuna baadhi ya viongozi wilayani humo bado wamelala wakidhani huu ni wakati wa kufanya siasa ilhali ilishakwisha mwaka 2015 na huu ni wakati wa kufanya kazi.
Hata hivyo, Diwani wa Loiborsiret (Chadema), Ezekiel Lesenga ‘Mardadi’ alisema mtu yeyote ana uhuru wa kujiunga na chama chochote anachokipenda.
Alisema watu hao walijiunga na Chadema kwa hiari na wamerudi CCM kwa kuamua wenyewe, hivyo yeye hana kizuizi wala hataki kumng’ang’ania mtu.
“Bado Chadema ipo imara Simanjiro hao wanaokwenda wacha waende watarudi tena, mimi sijawafuata naendelea kuwa Chadema,” alisema Mardadi.
Katika hatua nyingine, Mnyeti alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo, Zephania Chaula kuhakikisha anamaliza mgogoro wa uongozi wa kijiji hicho.
“Siku nne rudi hapa ufanye mkutano wa kijiji kama hawa wajumbe wa serikali ya kijiji ndiyo tatizo fuateni utaratibu waondoke uchaguzi ufanyike upya,” aliagiza Mnyeti.
Pia, alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Yefred Myenzi kuhakikisha uchaguzi mdogo kujaza nafasi za uenyekiti utakaofanyika Machi 25 ujumuishe na kijiji hicho.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: