Baada ya kuwepo kwa taarifa za kuugua kwa Mbunge mteule wa Jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, Muungwana Blog iliamua kufunga safari hadi ofisini kwake ili kuthibitisha juu ya yale yanayoenezwa kuhusu afya yake.

Kumekuwepo na taarifa za kusumbuliwa na ugonjwa wa kichwa ikiwa ni pamoja na kuanguka mara kwa mara, kupoteza fahamu lakini Ofisi ya Mbunge huyo imekanusha na kuziita taarifa hizo kuwa ni uzushi ambao unaenezwa na watu wasiomtakia mema Mbunge huyo.

Mbarouk Mchopanga ambaye ni Msaidizi wa Mbunge aliiambia Msumbanews  kuwa Mtulia yupo imara kiafya na hana tatizo lolote la kiakili kama inavyoenezwa na anaendelea vizuri na majukumu yake ya kisiasa na kwa sasa anasubiri kuapishwa bungeni Aprili 3, mwaka huu.

" Hata sisi tumezisikia habari hizo lakini niwahakikishie wananchi wa Kinondoni na Watanzania kwa ujumla kwamba Mbunge wao ni mzima wa afya na anahudhuria ofisini kila siku na hata jana alikuepo kwenye kikao cha CCM Makumbusho.

" Niwaombe watanzania watupilie mbali uzushi huo ambao unaenezwa na watu ambao hawaitakii mema Kinondoni na Mbunge wao, niwasihi sana wasiwe wanapokea taarifa ambazo hazijathibitishwa, Mtulia akiwa mgonjwa wananchi lazima wafahamu maana suala la ugonjwa sio la kuficha ni jambo ambalo litajulikana tu, hivyo niwatoe wasiwasi na Aprili 3 watashuhudia mbunge wao akiapishwa bungeni," amesema Mchopanga.

Kuhusu kutoonekana kwake mara kwa mara, Mchopanga alisema kwa sasa ni ngumu kuonekana kwa sababu bado hajaapishwa lakini hiyo haina maana kuwa anaumwa.

" Ni jambo ambalo linashangaza kidogo watu kumuongelea vibaya Mbunge kwa sababu eti hajafanya press na wandishi au hajaonekana hadharani ila wanasahau kuwa siku ile ya kutangazwa kwa matokeo Mtulia alikesha pale kituoni Biafra na asubuhi alipata wasaa wa kuzungumza na wandishi baada ya kutangazwa mshindi, wenye wasiwasi na afya yake wasubiri vikao vya Bunge vianze waone kama hatoapishwa na kuhudhuria Bungeni.

Kumekuepo na taarifa ambazo zinasambaa mitandaoni kuhusu afya ya Mbunge huyo mteule tangu kutangazwa kwa matokeo ya Ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni ambapo Mtulia aliibuka mshindi mbele ya Mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Salum Mwalimu.

Msumbanews Blog bado inaendelea kufuatilia kwa undani ikiwa ni pamoja na kumpata mwenyewe Mtulia ili aweze kuzungumzia taarifa hizo zinazoeneza ugonjwa wake na hatua gani anaweza kuwachukulia wale ambao wanasambaza taarifa hizo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: