Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), imevipika marufuku takribani vyuo 163 vilivyopo nchini Tanzania kuacha kuwafanyia udahili wa masomo wanafunzi wanaotarajia kujiunga na elimu ya juu kwa mwaka 2018 kutokana na kutokidhi vigezo.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Udahili Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi, Twaha Twaha leo (Machi 23, 2018) wakati walipokuwa wanazungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na kusema baraza linawataka waombaji wa nafasi za mafunzo kwa ngazi za Astashahada na Stashahada kwa muhula wa masomo wa Machi/Aprili, 2018 kuomba kwenye vyuo vilivyokidhi ubora ambavyo vimeorodheshwa kwenye tovuti ya baraza na sio vinginevyo.
"Baraza lilifanya uhakiki 'academic audit' kwenye vyuo vyote ambavyo vimesajiliwa na baraza ili kuweza kujiridhisha kuona kwamba vina sifa na mambo mbalimbali ambayo yanahusika na utoaji wa taaluma. Katika uhakiki huo, Baraza lilibaini kuwa baadhi ya vyuo vilikidhi viwango vya ubora kwa mujibu wa taratibu za Baraza.  Hata hivyo, baadhi ya vyuo vilibainika kuwa na changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri ubora wa elimu na mafunzo yanayotolewa", amesema Twaha.
Pamoja na hayo, Twaha ameendelea kwa kusema "kufuatia zoezi hilo vyuo vyote vilivyobainika kuwa na mapungufu vilitaarifiwa na kutakiwa kurekebisha mapungufu yaliyobainishwa kabla ya kuendelea na udahili wa wanafunzi kwa mwaka mpya wa masomo 2018/2019".
Kwa upande mwingine, Twaha amesema kuwa udahili wa muhula wa Machi/Aprili, 2018 hauhusishi programu zote za kada ya Afya na Ualimu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: