Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inajitahidi kujenga na kutanua vituo vya Afya ikiwa na lengo la kupunguza msongamano kwenye hospitali za Wilaya.
Makamu wa Rais ameyasema hayo jana wakati wa kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa kituo cha Afya Ihongole kilichopo mjini Mafinga.
Makamu wa Rais ambaye yupo kwenye ziara ya kuhamasisha shughuli za kimaendeleo mkoani Iringa ambapo jana alitembele wilaya ya Mufindi na kuweka mawe ya msingi katika miradi miwili ikiwa mmoja ni wa kujenga maabara ya kisasa na madarasa na kidato cha tano na cha sita katika Sekondari ya Mgololo na upanuzi wa kituo cha Afya cha Ihongole kilichopo Mafinga.
Akiwahutubia wananchi waliojitokeza kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la Upanuzi wa kituo cha Afya Ihongole , Makamu wa Rais alisema katika kila kituo cha afya kinachopanuliwa ama kujengwa Serikali imezingatia huduma za mama na mtoto ili kupunguza vifo vya akinamama na watoto, kuborsha huduma za upasuaji .
Serikali imetoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya upanuzi wa kituo hicho na kutumia mafundi wa kawaida kujenga ilikuweza kusaidia kutoa ajira kwa vijana zaidi wa eneo husika.
Makamu wa Rais amezitaka halmashauri zisimamie utoaji na matumizi ya fedha wanazotoa kwa Vijana asilimia 5 na Wanawake asilimia 5 ili kuleta tija kwenye shughuli za maendeleo.
Makamu wa Rais alisema “Tunapozungumzia uchumi wa viwanda lazima tuwaandae Vijana tangia wadogo, tuhakikishe wanafundishwa yale yanayohitajika”.
Makamu wa Rais aliwaambia wakazi wa Mafinga, watakapokuja tena kwenye kampeni watawataka wananchi waseme Serikali yao imewafanyia nini.
Mapema jana Makamu wa Rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa maabara na madarasa ya kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari Mgololo, ujenzi ambao utagharimu shilingi milioni 450 za kitanzania chini ya ufadhili wa kiwanda cha Mufindi Paper Mills.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: