Bila kujali ni kiasi gani walitunza, wateja kwenye benki tano zilizotangazwa kufilisika, wataambulia si zaidi ya Sh1.5 milioni ya amana zao kwa mujibu wa sheria.

Jana, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu aliwaaga Watanzania baada ya kuiongoza taasisi hiyo muhimu kwa uchumi wa Taifa kwa miaka 10 mfululizo na kueleza kuwa tayari benki zilizofilisika zimekabidhiwa katika Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kwa taratibu za kisheria.

Kaimu mkurugenzi wa bodi hiyo, Richard Malisa alimhakikishia Profesa Ndulu kuwa taratibu za malipo hayo zitafanyika haraka iwezekanavyo huku kiwango cha juu kitakacholipwa kwa wateja kikiwa ni Sh1.5 milioni.

“Mwenye amana za Sh100,000 atalipwa kiasi hicho na mwenye Sh50,000 atalipwa hiyo ila kiwango cha mwisho ni Sh1.5 milioni. Kwa hiyo, kama wewe una Sh5 milioni utakacholipwa ni Sh1.5 milioni,” alisema.

Taasisi tano zilizotangazwa kufilisiwa ni Benki ya Wanawake Convenant na Efatha. Nyingine ni benki za wananchi; Njombe na Meru pamoja na Benki ya Wakulima Mkoa wa Kagera (KFCB) ambazo zinaungana na FBME, Twiga Bancorp na Benki ya Wananchi Mbinga zilizofilisika na kufutiwa leseni mwaka jana.

Nyingine tatu zimewekwa chini ya uangalizi ambazo ni Benki ya Ushirika Kilimanjaro, Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) na Benki ya Wananchi Tandahimba ambazo, endapo zitashindwa kukidhi vigezo, baada ya muda, nazo zitafilisiwa.

Kuhusu athari za kufungiwa na kufilisiwa kwa benki hizo Profesa Ndulu alisema jumla ya amana za benki zote nane ni Sh67.6 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 0.38 ya benki zote 58 zilizopo nchini hivyo kutokuwa tishio.

“Hakuna athari zozote za kiuchumi zinazoweza kujitokeza kutokana na kufungiwa kwa benki hizi. Lakini, endapo tungeziacha ziendelee kujiendesha hivyohivyo, madhara yake yangekuwa makubwa,” alisema.

Profesa Ndulu alitaja sababu za benki ndogo kutofanya vizuri kuwa ni kutokana na kukosa mtaji, wigo mdogo wa biashara, ukubwa wa bodi zinazozisimamia pamoja na gharama kubwa za uendeshaji.

“Tumewashauri waungane, wawe shirikisho halafu hizo benki nyingine ziwe matawi kusaidia mfumo wao wa undeshaji uwe mmoja kupunguza gharama lakini utekelezaji umekuwa mgumu,” alisema.

Mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Benki za Kijamii (Cobat), Lukwaro Senkoro alikiri kupewa ushauri huo na BoT lakini akasema muda haukuwa rafiki kwao kuutekeleza ingawa hatua za makusudi zilichukuliwa.

Alisema katika jitihada hizo za kukamilisha mchakato wa kuziunganisha benki za wananchi, chama hicho kilianza kwa kukutana na bodi za wakurugenzi wa benki husika ambazo ziliafiki ushauri huo na kuahidi kwenda kuzungumza na wanahisa wao.

“Huko ndiko kulikosumbua,” alisema. “Benki sita zilikubali kuungana lakini tatu wanahisa wake wanahitaji muda wa ziada kufikiri kuhusu suala hilo,” alibainisha.

Alisema kwenye mkakati wao, walishafanikiwa kumpata mwekezaji atakayeiwezesha Benki ya Taifa ya Wananchi ambayo ingeanzishwa lakini baada ya benki tatu kutangazwa mufilisi, mchakato huo utakuwa umefika mwisho.

Alisema ushauri wa BoT ni wazo jipya lililohitaji kujadiliwa na wadau kabla ya kuridhia kuungana na kujiendesha chini ya mwamvuli mmoja hivyo kuhitaji muda wa kutosha wa uelimishaji.

“Ushauri ulitolewa Juni na tulipewa mpaka Oktoba tuwe tumekamilisha taratibu ili Novemba mwaka jana tuungane. Tumepambana mpaka mwisho lakini hatujafanikiwa. Kwa sasa mpango huo hautekelezeki,” alisema kwa masikitiko.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: