SHAHIDI katika kesi inayomkabili Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Chadema) na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga, ameiambia mahakama alivyonasa kauli za mbunge huyo kwa kumrekodi.


Kesi hiyo jana iliendelea kunguruma kwa siku ya pili mfululizo huku shahidi huyo akieleza Sugu alivyoingia katika mtego huo bila kujijua. 

Shahidi huyo namba tano. Joram Magova, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika Ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Mbeya, alidai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya kuwa Desemba 30, mwaka jana, watuhumiwa hao walitoa maneno ya fedheha kuhusu Rais.

Alidai kuwa aliagizwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO), Modestus Chambu, kwenda katika eneo la Shule ya Msingi Mwenge kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa mkutano huo.
Alidai kuwa alikwenda katika mkutano huo akiwa na kifaa cha kunasia sauti (tape recorder) kwa ajili ya kuchukua ushahidi na kwamba alipofika katika eneo hilo, alikaa umbali wa kati ya mita 20 na 30 akaendelea kunasa sauti kwa kutumia kifaa hicho.

Aliyanukuu baadhi ya maneno yanayodaiwa kutamkwa na watuhumiwa akidai hata yeye mwenyewe yalimuumiza kwa madai kuwa yalikuwa yanamfedhehesha Rais John Magufuli na kuhatarisha amani ya wananchi waliohudhuria mkutano huo.

“Katibu Masonga alisema watu wanauawa mchana na kutupwa kwenye viroba mchana kweupe, wanatekwa mchana kweupe, Magufuli anaona njia pekee ya kuwatawala Watanzania ni kuwaua. Maneno haya yalikuwa si ya staha dhidi ya Rais,” alidai Magova na kuongeza:
“Mbilinyi alisema huwezi kupendwa kwa kumweka Lema ndani, ‘kumshuti’ (Tundu) Lissu, kumteka Roma na Ben Saanane ambaye hajulikani alipo mpaka sasa.”

Hata hivyo, alidai kuwa alishuhudia baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kutopendezwa na maneno yaliyotamkwa na viongozi hao, hivyo kuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani.
Pia alidai kuwa mkutano huo ulimalizika saa 12:12 jioni, lakini yeye aliendelea kubaki eneo hilo kwa ajili ya kutathmini na kutoa taarifa ya kilichotokea kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mbeya na Ofisi ya Upelelezi Mkoa.

Aliongeza kuwa ilipofika saa 12:30 jioni aliwasiliana na mtunza vielelezo wa Ofisi ya Upelelezi Mkoa, Daniel Masanja, ambaye ndiye shahidi namba nne, akimtaka wakutane ofisini ili amkabidhi kifaa cha kunasa sauti mpaka kitakapohitajika tena.
Alidai kuwa Januari 2, 2018 baada ya Mbilinyi na Masonga kukamatwa kwa ajili ya kuhojiwa, alimwagiza mtunza vielelezo, Masanja alete kinasa sauti kwa ajili ya kusikiliza ili kuwaridhisha watuhumiwa.

Shahidi huyo aliiomba mahakama isikilize sauti hizo zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye kinasa sauti, hali ambayo alidai ilisababisha kuibuka kwa mabishano ya kisheria baina ya mawakili wa Jamhuri na wa utetezi. Upande  wa Jamhuri walikuwa wanataka sauti zisikilizwe na upande wa utetezi ukipinga.
Baada ya mabishano hayo Hakimu Mkazi Michael Mteite, aliahirisha kesi hiyo mpaka leo na uamuzi wa kusikilizwa au kutosikilizwa sauti hizo utatolewa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment:

Back To Top