Na Mathias Canal, Dar es salaam
Uongozi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) umetakiwa kutoa maelezo kwa serikali katika kipindi cha muda mfupi kueleza sababu za kuendelea kusalia kuwepo kwa shirika hilo kutokana na kukosa umakini katika utendaji.
 
Kauli ya kuchukizwa na utendaji wa Shirika hilo imetolewa Leo 16 Januari 2018 na Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko Wakati akizungumza na Uongozi pamoja na watumishi wa Shirika hilo Mtaa wa Upanga Jijini Dar es salaam.
 
Mhe Biteko alisema kuwa serikali ilikuwa na makusudi mazuri kufuatia mabadiliko ya Sera za kiuchumi katika miaka ya 1980 kwa STAMICO kuwekwa kwenye orodha ya mashirika yanayotakiwa kubinafsishwa na hatimaye kubinafsishwa rasmi mwaka 1996 lakini katika kipindi chote cha utendaji hakuna msaada wowote ambao Shirika hilo limeipatia serikali zaidi ya kuingiza hasara maradufu.
 
Alisema kuwa pamoja na STAMICO kuwa na jukumu la kuendeleza migodi ya Madini na kufanya biashara za Madini ikiwemo mradi wa dhahabu wa STAMIGOLD uliopo Biharamlo Mkoani Kagera na Mgodi wa Makaa ya Mawe KABULO uliopo Mkoani Ruvuma lakini Taasisi hiyo imeshindwa kuendeleza migodi kwa ufanisi huku wachimbaji wadogo wakisalia kuwa katika uduni wa mbinu rafiki na tija katika utendaji kazi wao.
 
Alisema kuwa Shirika hilo linapaswa kutafakari kwa umakini
utendaji wake kwani limeongeza hasara kwa serikali ya deni la shilingi Bilioni 1.77 hivyo serikali haiwezi kuendelea kusalia kuwa na Shirika linalozalisha madeni kuliko matokeo makubwa na faida.
 
Aliongeza kuwa wataalamu wote katika sekta ya Madini wanapaswa kutambua kuwa biashara ya Madini ni zaidi ya kutoa leseni hivyo watambue kuwa kuna kila sababu ya kuwa na matumizi bora ya mapato na kutazama namna bora ya kuifanya sekta ya Madini kuchangia asilimia 10% ya pato la Taifa.
 
Mhe Biteko alisema kuwa imani bila matendo ni uduni wa fikra hivyo kuwa na cheo kikubwa serikalini halafu uzalishaji ni mdogo ni kipimo halisi cha utendaji wa mazoea walionao watumishi wengi ambao wamekosa uzalendo na bidii katika utendaji kazi.
 
Alisema kuwa serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli imekusudia kusimamia vyema rasilimali za wananchi hivyo watendaji katika sekta mbalimbali wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kumsaidia Rais Magufuli katika kuteleleza adhma ya serikali.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: