Wenyeviti hao wameliambia gazeti hili kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kuona vitendo hivyo vinazidi kukithiri, wanaitaka Tume ya Maadili iingilie kati.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mavurunza, Josephat Nehemia alisema mkuu huyo wa wilaya amekuwa akiwanyanyasa wenyeviti wa mitaa kwa kuagiza askari kuwakamata bila kuwaeleza makosa yao.

Nehemia alisema kwa muda mrefu amevumilia uonevu huo ila kwa sasa ameona awasilishe malalamiko yake katika sekretarieti ya maadili ili yaweze kushughulikiwa.

“Anachokifanya DC ni ukiukwaji wa maadili ya uongozi, kiongozi huwezi kuwa unasikiliza maneno bila kuyafanyia uchunguzi unaagiza mwenyekiti awekwe ndani, tunawekwa mahabusu bila kuambiwa makosa yetu, suala hili sasa basi,” alisema.

Naye mwenyekiti wa mtaa wa Kimara Baruti, Aloyce Kinyonga alidai kuwa DC huyo alimtukana hadharani kwa kumuita mtu asiye na maana.

“DC akiwa kwenye mkutano mtaa wa Kilungule A alitamka mbele ya wananchi kuwa mimi sina nidhamu, ni mtu wa hovyo kosa langu likiwa ni kuandika barua kuhusu suala la umeme, nimeona nami nilete malalamiko yangu tume ili waone viongozi wasiozingatia maadili,” alisema.

Akizungumzia suala hilo, mwenyekiti wa mtaa wa Makoka, Emmanuel Akyoo alisema kitendo cha kuwekwa ndani bila kuambiwa kosa alilofanya kinamsababishia kushindwa kutekeleza majukumu yake.

“Nashindwa kufanya kazi vizuri, muda wote nakuwa na wasiwasi na ninaamini hatuwezi kuendelea kwa mtindo huu, lazima viongozi tufanye kazi kwa uhuru,” alisema.

Kauli ya DC

Kisare alisema wenyeviti wote waliowekwa ndani walikuwa na makosa na kwamba hafahamu sababu za kumtuhumu.

Alisema wenyeviti wote ambao amewachukulia hatua walikuwa na makosa mbalimbali ikiwamo ubadhirifu, ukiukwaji wa taratibu na uonevu kwa wananchi.

“Hao ni watu wanaotaka kufanya siasa, sisi hatuna muda wa porojo lengo letu ni kuleta maendeleo hivyo hatuwezi kuvumilia wanaotumia nafasi zao kama mtaji,” alisema.

Akitoa mfano mtaa wa Golani ambako mwenyekiti wake aliwekwa ndani kwa kosa la kukiuka mwongozo uliotolewa na manispaa kwa ajili ya kufanya urasimishaji.

“Manispaa imeweka mwongozo kwa kila kata kuwe na urasimishaji wa makazi na gharama ya mpimaji isizidi Sh260,000 yeye akaenda kuleta mtu wa kufanya kazi hiyo kwa Sh450,000, akawa anawaweka ndani watu waliokuwa wanapinga gharama hizo,” alisema. 
Share To:

msumbanews

Post A Comment: