Vigogo wa Chadema na CCM leo wataliteka Jiji la Dar es Salaam katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi jimbo la Kinondoni watakapokuwa wakiwanadi wagombea wa vyama hivyo.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe baada ya jana kuongoza uzinduzi wa kampeni za ubunge wa Jimbo la Siha, leo pia atakuwapo katika Viwanja vya Ali Mapilau, Mwanyamala kumnadi mgombea wa chama hicho Jimbo la Kinondoni, Salim Mwalimu.

Wakati Mbowe akiwa huko, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Mwigulu Nchemba atakuwa katika Viwanja vya Biafra, Kinondoni akimnadi mgombea wa CCM, Maulid Mtulia.

Kama ilivyokuwa kwa Mbowe, Dk Nchemba ndiye pia aliyezindua kampeni za uchaguzi za CCM katika jimbo la Siha.

Kama ilivyo Kinondoni, Siha nako unafanyika uchaguzi baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema Dk Godwin Mollel kuhamia CCM na kuteuliwa kugombea tena nafasi hiyo kupitia chama tawala akichuana vikali na mgombea wa Chadema, Elvis Mosi.

Mtulia naye alijiuzulu uanachama wa CUF hivyo kupoteza ubunge wa Kinondoni na kupitishwa na chama hicho tawala kuwania tena nafasi hiyo.

Uchaguzi huo utakaofanyika Februari 17, unatarajiwa kuwa na mpambano mkali kutokana na vyama 12 kujitokeza katika kinyang’anyiro hicho.

Jana, Mtulia alisema Dk Nchemba ndiye atakayekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, “Ingawa tayari tumeshaanza kampeni za ndani kwa maana ya kuzungumza na wanachama wa CCM katika kata 10, kesho (leo) ndio tunazindua rasmi.”

Katibu wa siasa na uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Simon Mwakifamba alisema shamrashamra za kampeni hizo zitaanza saa sita mchana na kuwataka wakazi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo.

“Hiki ni chama dume na imara, naomba watu wajitokeze kwa wingi,” alisema.

Mwakifamba alisema chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam kimeamua kuzigawanya kata 10 za Jimbo la Kinondoni kwa viongozi wa chama hicho kutoka wilaya tano za jiji hilo na kila wilaya imepewa kata mbili kwa ajili ya kufanya uhamasishaji kuhakikisha mgombea wao anashinda.

Leo Mbowe atazindua kampeni za Chadema Kinondoni akisindikizwa na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.

Mkurugenzi wa Itifaki Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema alisema hawakutaka kuzindua kwa pamoja kampeni za Siha na Kinondoni ili kutoa ushiriki mpana wa viongozi wake katika kila jimbo.

Mbali na Mbowe, viongozi wengine wanaotajwa kushiriki uzinduzi wa kampeni hizo ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

Lipumba CUF

Kesho, Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba atazindua kampeni za chama hicho jimbo la Siha atakapomnadi mgombea wa chama hicho, Tumsifuel Mwanry.

Kampeni Siha

Katika uzinduzi wa kampeni za Siha jana, Mbowe alisema wananchi wa jimbo hilo wangekuwa wamebebeshwa gunia la misumari kama Dk Mollel angeendelea kuwa mbunge.

Wakati Mbowe akieleza hayo, mgombea wa chama hicho, Mosi aliwaambia wananchi waliojitokeza katika uwanja wa Kituo cha Afya cha Ngarenairobi kwamba siku atakapoihama Chadema, wananchi wachome moto nyumba anayoishi.

Katika ufafanuzi wake, Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai alimshangaa Dk Mollel kujiuzulu kwa madai ya kumuunga mkono Rais John Magufuli na kusema angeweza kumuunga mkono kwa kufanya vyema kazi ya ubunge.

“Tunapokwenda kwenye uchaguzi huu sio tu tunaenda kumchagua mbunge. Tunakwenda kuleta mtu atakayelitetea jimbo hili. Tunaleta mtu asiye na bei. Tunaomba mtuamini,” alisema Mbowe huku wabunge wa viti maalumu wa chama hicho, Cecilia Paresso na Lucy Owenya wakisema adhabu pekee kwa wananchi dhidi ya Dk Mollel ni kumnyima kura.

CCM yanguruma Siha

Akizungunza katika mkutano wa kampeni wa kumnadi Dk Mollel na diwani wa Kashashi, Suzan Natai katika Viwanja vya Kashashi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rodrick Mpogolo alisema atafunga kwa maombi kwa siku saba ili kuwezesha ushindi wa kishindo.

Mpogolo alisema CCM ilikuwa na madiwani wanane wa kuchaguliwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Siha huku Chadema wakiwa tisa, lakini kutokana na madiwani watatu wa Chadema kujiuzulu anaamini watazinyakua kata zinazorudia uchaguzi na kufanikiwa kuiongoza halmashauri hiyo.

“CCM tunahitaji kura zote kwa mbunge na madiwani na ili kufanikiwa hili nitafunga kwa siku saba kuomba. Naamini Mungu ni mwema atatupigania na kutuwezesha kushinda, kuwaletea wananchi wa Siha maendeleo ya kweli,” alisema Mpogolo.

Akizungumza katika mkutano huo, Dk Mollel alisema wananchi walimchagua kuwa mbunge akiwa kwenye timu isiyo na uhakika lakini sasa amejiunga na timu ya ushindi katika maendeleo.

“Ndugu wananchi wa Siha, niwahakikishie kuwa hamtajuta kunichagua kwa sababu ndani ya miezi sita nitafanya maajabu ya maendeleo katika jimbo hili. Nitumeni ili nikawatumikie kwa uaminifu na kuwaletea maendeleo,” alisema.

Aliwaasa wananchi kuepuka siasa za kupigana na kumwaga damu kwa kuwa wagombea katika jimbo hilo wana haki sawa.

“Polisi mtuongoze kwa amani katika kipindi hiki cha kampeni bila kujali vyama vya siasa,” alisema
Share To:

msumbanews

Post A Comment: