Uongozi  wa timu ya Coastal Union ya Tanga(al maarufu Wagosi wa Kaya) umekataa ufadhili waliotafutiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, anayeshughulikia Mazingira na Muungano, January Makamba kwa madai kwamba kampuni aliyoitafuta kwa ajili ya ufadhili inajishughulisha na masuala ya Kamari.


Waziri Makamba alitafuta Ufadhili kutoka kampuni ya BIKO inayojihusisha na michezo ya kubahatisha ambayo ilikubali kuifadhili timu ya Coastal kwa kuingia nayo mkataba ambao utawezesha kulipa mishahara ya wachezaji pamoja na mahitaji mengine kwa kipindi cha mwaka mmoja.


Makamba alisema lengo la yeye kukubali kuwatafutia ufadhili ilikuwa ni kutaka kuinua kiwango cha soka pamoja na kuipa nguvu ili  iweze kupanda daraja timu hiyo iliyoporomoka kisoka.


Akizungumza kwa simu na mwandishi wa habari hii, Waziri Makamba alikiri  kuitafutia ufadhili timu hiyo ambao ungewawezesha kulipwa mishahara na mahitaji mengine kwa kipindi cha mwaka mzima.


imefahamika kuwa uongozi wa Coastal Union umekataa ufadhili huo licha ya kufanyika mazungumzo ya awali kwa ajili ya kuingia mkataba.


Ofisa Mtendaji Mkuu wa BICO, Charles Mgeta alisema kuwa taratibu za ufadhili zilikuwa zimekamilika na walipeleka fedha za awali zipatazo sh.15m/= kwa klabu hiyo kati ya fedha sh.50m/= zilizokubaliwa kwa matumizi ya mwaka mzima.

Mgeta alisema kwamba licha ya kupeleka fedha za awali pia walipeleka jezi 30 kwa ajili ya timu hiyo na kuahidi kutengeneza jezi 30 nyingine.


Ofisa Mkuu huyo alisema baada ya kutokea sintofahamu juu ya ufadhili huo kutoka CoastalUnion, kampuni ya BIKO imewataka viongozi wa klabu hiyo kurudisha fedha walizopokea kutoka kwao.


Hata hivyo, uongozi wa Coastal Union umethibitisha kupokea fedha zipatazo shs.15m= kutoka BIKO na kwamba wanachofahamu ni kwamba wanaendelea na mazungumzo na kampuni hiyo ili waweze kupata suluhu, ingawa hakufafanua zaidi.


Mwenyekiti wa Coastal Union, Stephen Mgutto alisema kwamba klabu yake ilipendekeza ipewe ufadhili wa shs. 50m/= badala ya shs. 30m/= ambazo walitajiwa.


Alieleza kuwa kushindwa kufikiwa muafaka wa shs.50m/= ulifanya uongozi wa klabu hiyo kutotaka kuendelea na mkataba na kampuni hiyo.Katibu wa Kamati Maalum ya mashindano na Usajili, Salim Bawazir alisema kuwa Waziri Makamba amekuwa mfadhili wa timu hiyo kwa muda mrefu na alitaja baadhi ya misaada iliyotolewa naWaziri Makamba kwa Coastal Union kuwa ni pamoja na kugharamia kambi ya timu hiyo wakati wakijinoa  kwa muda wa majuma mawili kwa kutoa shs.2m/=.


“Mheshimiwa, ametugharamia kuweka kambi ambayo ilihusisha chakula na vitu vingine,  ambapo Mohamed Enterprises naye aliisaidia timu kwa kutoa vyakula vyenye thamani ya shs.2m/=”. Alisema Bawazir.


Makamba alisema kuwa ametumia karibu shs.6m/= kuisaidia timu hiyo kwa matumizi yao kuanzia mwaka jana.


“Nimewalipia mara kadhaa mahitaji yao yanayofikia shs.6m/=”, alisema Waziri huyo.


Alisema amesikia tetesi za mtafaruku baina ya viongozi kuhusu upokeaji wa msaada huo na kueleza kuwa amesikitika sana. "Iwapo msaada huo hauhitajiki, tutawapa wengine wanaohitaji”, alisema Makamba na kuongeza amekuwa akisaidia michezo kwa muda mrefu na mwaka jana alipewa ngao ya shukurani na timu ya Majimaji ya Songea kwa sababu aliwasaidia na wakafanikiwa.


"Viongozi hao wanajua kabisa kwamba mara kadhaa nimelipia mahitaji mbalimbali ya klabu ingawa kipato changu ni kidogo. Nimeenda kambini na kufanya mkutano na wachezaji kuhusu hali zao. Nikihesabu tangu mwaka jana ni fedha nyingi," alisema.


Alieleza kuwa kuna kipindi timu ilipitia Iringa  na akalazimika kuwaomba marafiki zake wa Iringa wawapokee, kuweka mafuta na kuwapa chakula na malazi.


Alisema anatumaini kuwa mzozo huo utamalizwa kwa ustawi wa soka la Tanga.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: