Kilimanjaro Stars imeshindwa kutamba dhidi ya ndugu zao Zanzibar Heroes baada ya kukubali kichapo cha magoli 2-1 katika uwanja wa Kenyatta uliopo eneo la Machakos Kenya.

Kilimanjaro Stars imeanza kupata goli dakika ya 28 lililofungwa na Nahodha wa timu hiyo Himid Mao, baada ya gonga nzuri na Dany Lyanga .

Goli la Himid Mao limedumu hadi kipindi cha kwanza kinaisha, kilipoanza kipindi cha pili dakika ya 66  "super sub" Kassim Hamis amepata goli la kusawazisha, wakati goli la ushindi lilifungwa dakika ya 78 na Ibrahim Ahmada aliyepokea pasi safi kutoka kwa Suleiman Selembe.

Baada ya mchezo huo mchezaji bora wa mechi  Ibrahimu Ahmad  amekisifu kikosi chake cha Zanzibar Heroes huku akimsifia kocha wake Hemed Morocco kwa kuwahamasisha.

'Mwalimu ametuhamasisha na alitueleza kabisa kuwa tutashinda mchezo huu, kweli tumefanya hivyo, mabadiliko aliyoyafanya yameleta alama tatu leo", amesema Ibrahim Ahmd.

Zanzibar wamefikisha alama 6 ikiwa kileleni mwa kundi "A" ikifuatiwa na wenyeji Kenya, Zanzibar inaogoza kwa wingi wa magoli.

Katika kundi hilo imebakia michezo miwili  Kilimanjaro Stars inatakiwa ishinde   michezo yote ili kujiweka vizuri katika hatua inayofuata.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: