SeeBait
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema uwepo wa uchumi imara na unaokua kwa kasi ni miongoni mwa vigezo vinavyochangia ukuaji wa haraka wa sekta ya fedha nchini.
 
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Desemba 21, 2017) wakati akizindua Mpango wa Pili wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha katika ukumbi wa Benki Kuu jijini Dar es Salaam.

Akizindua mpango huo unaotarajiwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2018 hadi 2022, Waziri Mkuu alisema uwepo wa miundombinu muhimu iliyojengwa na inayojengwa na Serikali; na sekta binafsi katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya vijijini; na ongezeko la watumiaji wa mitandao ya simu na huduma za mawasiliano ni kati ya fursa nzuri iliyotajwa kwenye mpango huo.

“Kati ya fursa nzuri iliyotajwa kwenye mpango huo ni uwepo wa uchumi imara na unaokua kwa kasi. Tukijenga vizuri juu ya misingi hii tunaweza kupiga haraka hatua za maendeleo katika sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla wake,” alisema.

Alisema ameupitia mpango huo na kubaini kuwa umeainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi hii katika harakati zake za kuongeza matumizi ya huduma za kifedha. Hata hivyo, Waziri Mkuu alikiri kuwa mpango huo umeainisha fursa ambazo zinaweza kutumika ili kukabiliana na changamoto hizo na hatimaye kuongeza matumizi ya huduma za kifedha.

“Changamoto zilizoainishwa ni pamoja na kuimarisha utawala wa matumizi ya fedha taslimu kwa ajili ya malipo badala ya matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya malipo; kukosekana kwa utambulisho wa kipekee (unique identification) kwa Watanzania walio wengi; uhalifu kwa njia za mtandao (cyber-crime); kukosekana kwa mifumo madhubuti ya taarifa za kutosha za watumiaji wa huduma za fedha na dhamana zao; na uelewa mdogo wa masuala ya kifedha,” alisema.

Aliwataka wajumbe wa Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za kifedha waaandae mpango mahsusi wa kutoa elimu vijijini kuhusu faida na umuhimu wa huduma jumuishi za kifedha Tanzania, na akasisitiza kuwa kipaumbele kitolewe kwa makundi maalum ya vijana na wanawake.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema wataalam wa uchumi duniani wanaeleza kwamba jamii ambayo imejijengea utamaduni wa kujiwekea akiba katika asasi za kifedha ina fursa kubwa ya kupata maendeleo endelevu na ya haraka.

“Hii ni kwa sababu uwekaji akiba ndiyo kiini na nguzo ya uwekezaji wa miradi ya maendeleo, na bila uwekezaji wa miradi ya maendeleo, hakuna maendeleo. Nchi zote zilizoendelea zimejijengea utamaduni huu wa wananchi wake wa kujiwekea akiba,” alisisitiza.

Alitoa wito kwa wajumbe hao kuhakikisha kuwa mpango huo unajikita zaidi katika kuimarisha utamaduni wa Watanzania kujiwekea akiba kwa kila aina ya mapato ambayo mwananchi anapata, iwe katika kilimo au biashara au ufugaji au uvuvi au shughuli nyingine yeyote anayofanya ya maendeleo.

“Taarifa ya Mpango wa Pili wa Huduma Jumuishi za Kifedha inaonyesha kuwa asilimia kubwa ya Watanzania (watu wazima) wanamiliki simu za mkononi na wanatumia simu hizo kufanya miamala ya kifedha. Kwa msingi huo, nashauri kuwepo kwa ushirikiano wa karibu baina ya wadau wa taasisi za fedha na wadau wa TEHAMA ili kuimarisha matumizi na mtandao wa kifedha vijijini ili iwe kichocheo cha uchumi,” alisema.

Mapema, Gavana wa Benki Kuu, Prof. Benno Ndulu alisema matokeo ya tathmini iliyofanyika yanaonyesha kwamba wananchi walio karibu na huduma za fedha wameongezeka kufikia asilimia 86 mwaka 2017 ya Watanzania (watu wazima) ikilinganishwa na asilimia 29 ya mwaka 2012.

Pia alisema Watanzania wanaotumia huduma za fedha hasa kupitia asasi za kifedha na mitandao ya simu wameongezeka kutoka asilimia 17 mwaka 2009 hadi asilimia 11 mwaka 2006, na hadi sasa (2017) takwimu zinaonyesha kwamba wananchi asilimia 65 wanatumia huduma za kifedha nchini.

“Kutokana na mafanikio haya makubwa, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika na ya sita duniani kwa kuweka mazingira bora ya utoaji na upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dk, Charles Kimei alisema wenye mabenki wana haja ya kubadili mtazamo na kujikita kwenye ngazi ya chini ambako kuna watumiaji wengi zaidi.

“Wenye kampuni za simu wameonyesha kuwa inawezekana kufikisha huduma kwa watu wa chini kupitia simu zao, nasi tukitumia vifaa hivyo tunaweza kuwafikia wananchi wengi kwa kuwapa huduma zetu,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa ngazi zote wakiwemo wa mikoa, wilaya na wabunge walifanye suala la uwekaji akiba liwe ajenda kuu ya mikutano yao kwa kuwaelezea wananchi umuhimu wa suala hilo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, DESEMBA 21, 2017   
Share To:

msumbanews

Post A Comment: