Naibu waziri wa maji na umwagiliaji Jumaa Aweso akimsikiliza mwananchi wa kijiji cha Bankolo kilichopo wilaya ya Bahi Esther Matonya aliyesimamisha msafara wake akiwa katika ziara wilayani humo na kueleza adha ya maji wanayoipata.

NAIBU waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso amewataka wakandarasi wa maji hapa nchini  kufanya kazi kwa bidii ili  maji safi na salama yapatikane na kuweza kufikia azma ya serikali ya awamu ya tano ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani kwa kuhakikisha maji mijini yanapatikana kwa asilimia 95 na vijijini asilimia 85 ifikapo 2020.

Maagizo hayo ameyatoa jana Wilayani Bahi  Mkoani Dodoma, wakati  akikagua chanzo cha maji cha Mkakatika,eneo la tanki la maji,kituo cha kuchota maji cha wananchi kilichopo katoka mradi wa maji wa halmashauri hiyo na mradi wa maji wa kijiji cha Mchito miradi ambayo kukamilika kwake itaongeza  upatikanaji wa maji hadi asilimia 48.73 kutoka asilimia 16 iliyopo sasa.
"Uhandisi wa maji maana yake maji yapatikane, wananchi hawataki kusikia mambo ya dizaini,upembuzi wala usanifu wanataka maji, fanyeni kazi watu wapate maji na sio vinginevyo"" Alisema Aweso na kuongeza kuwa 

"Ndugu zanguni mi unaibu waziri bado nautaka hivyo sitokubali kutumbuliwa,kabla sijatumbuliwa mimi nitakutumbua wewe timizeni majukumu yenu,"alisisitiza Aweso
Alisema serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha wilaya ya Bahi inapata maji ambapo katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 jumla ya shilingi  bilioni moja zimetengwa.
"Katika kuhakikisha mkoa wa Dodoma unakuwa na maji ya uhakika tumeamua kutumia bwawa la Farkwa kwa ajili ya kusambaza maji katika wilaya ya Chemba,Bahi na Dodoma mjini,ndugu zangu unapobebwa kiuno kikaze,ukikilegeza utaanguka,nawaomba mtunze miradi ya maji,"alisema Aweso.
ata hivyo Naibu waziri amemtaka mkandarasi wa maji Deus Mchele kuhakikisha ifikapo novemba 18 mwaka huu miradi yote ya maji iliyopo katika majaribio iwe imekamilika na kukabidhiwa kwa wananchi na sambamba na kuziba bomba linalovuja ambalo linapeleka maji kwenye tenki.

Akiwa njiani kuelekea kijiji cha Mchito Aweso alisimamisha msafara wake kijiji cha Bankolo na kuwasikiliza wananchi waliosimama kando ya barabara ambapo alipokea changamoto ya ukosefu wa maji na kuahidi kuondoa changamoto hiyo kama serikali ya awamu ya tano chini ya rais John Magufuli  ilivyoahidi.

Wakizungumza baadhi ya wanachi Abeid Juma aliempongeza Rais Magufuli na serikali yake kwa kuonyesha dhamira ya kutatua shida ya maji iliyokuwa inawafanya waamke alfajiri na kulala usiku sana hali iliyoleta changamoto katika ndoa zao.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo  Sosthenes Mpandu alimshukuru naibu waziri kwa ziara yake inayolenga kutatua tatizo la maji ambapo kwa sasa wananchi wa Bahi wananunua dumu moja shilingi mia tano hadi mia sita.
"Mh Aweso ziara yako imeleta manufaa,umetuonyesha na kudhihirisha kuwa rais hakufanya makosa katika kukuteua unaendana na kauli mbiu yake ya hapa kazi tu,,tunashukuru na kukuomba tena utukumbuke wilaya ya Bahi,"alisema makamu mwenyekiti.

Mhandisi wa Maji wa wilaya ya Bahi Deus Mchele akitoa maelezo ya mradi wa kijiji cha Mchito mbele ya naibu waziri wa maji na umwagiliaji Jumaa Aweso.

Naibu waziri Wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa Kijiji cha Mchito alipokuwa katika ziara yake wilayani Bahi pamoja nae yupo makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo Sosthenes Mpandu.
 
Share To:

msumbanews

Post A Comment: