TANGA. Waajiri wa sekta binafsi wametakiwa kuzingatia wajibu wao wa kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati ili kuwawezesha wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kupata mafao yao kwa mujibu wa sheria.
Wito huo umetolewa tarehe 8 Mei 2025 jijini Tanga na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Bi. Mwamini Malemi, wakati akizindua rasmi Mkutano wa 54 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mfuko huo.
Bi. Malemi amesema michango ya waajiri ni uti wa mgongo wa uendeshaji wa Mfuko, hivyo kucheleweshwa kwake kunaathiri moja kwa moja ustawi wa wanachama na ufanisi wa utoaji huduma za mafao.
“Naomba nitumie nafasi hii kuwaasa waajiri wote kuhakikisha wanawasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati. Hili si jambo la hiari bali ni wajibu wa kisheria unaolenga kulinda haki za wafanyakazi”, amesisitiza Bi. Malemi.
Ameongeza kuwa, NSSF inaendelea kutoa huduma bora na endelevu kwa wanachama wake kwa kuzingatia misingi ya uadilifu, uwajibikaji na matumizi ya teknolojia ili kuongeza uwazi na ufanisi katika shughuli za kila siku.
Akizungumza kuhusu mafanikio ya Mfuko, Bi. Malemi amesema NSSF imeendelea kuwa taasisi ya mfano katika sekta ya hifadhi ya jamii kwa kuimarisha mifumo ya TEHAMA, kuongeza kasi ya uandikishaji wanachama, kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato na kufanya uwekezaji wenye tija.
Kampuni ya Mamba Minerals Ltd yenye Leseni ya uchimbaji Madini adimu (Rare Earth Elements) imesema itaanza ujenzi rasmi wa Mgodi huo Disemba,2025 na uzalishaji wa kwanza kufanyika mwisho wa mwaka 2026.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma wakati wa kikao kati ya Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde na Viongozi wa Kampuni za Mamba Minerals na Shenghe Ltd.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Mwenyekiti wa Kampuni ya Mamba Minerals Ndg.Russell Scrimshaw amesema Kampuni hiyo imeitikia wito wa serikali wa kuhakikisha uzalishaji wa madini unaanza mapema iwezekanavyo kamba ambavyo Waziri wa Madini amesisitiza na hivyo kwa kushirikiana na wabia wenza Kampuni ya Shenghe watahakikisha ujenzi wa mgodi unaanza mapema mwezi Disemba 2025 na uzalishaji wa kwanza kufanyika mwishoni mwa mwaka 2026.
Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya Shenghe Ndg. Quangan Wang amesema Ujenzi wa mgodi huo pia utaenda sambamba na ujenzi wa Kiwanda cha kuchenjua na kusafisha madini hayo pamoja na ujenzi wa Mtambo wa kuzalisha umeme wa kuanzia megawati 10-12 kwa matumizi ya mgodi na jamii inayozunguka mradi.
Madini adimu haya hutumika kwenye kutengeneza vifaa vya kieletroniki,vifaa vya uzalishaji umeme kutumia upepo,Mota za magari ya umeme na Vifaa vya hospitali.
Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amepongeza hatua ya Kampuni hiyo kuzingatia maelekezo ya serikali ya kuanza uendelezaji wa mgodi wa madini adimu kwa uharaka na kuendelea kusisitiza kwamba wamiliki wote wa Leseni za kati na Leseni kubwa kuhakikisha wanaanza shughuli za uchimbaji wa madini ndani ya miezi 18 ambayo imetamkwa kwenye Sheria ya Madini Sura ya 123.
📌 Asema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa elimu
📌 Asema Afrika lazima iendelee kuimarisha mazingira wezeshi kwa kampuni bunifu za kidigitali
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza wadau wa elimu barani Afrika kuendeleza mkakati na ushirikiano utakaowezesha mageuzi ya kidigitali katika sekta ya elimu.
Dkt. Biteko ametoa rai hiyo Mei 8, 2025 jijini Dar es salaam wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano la 18 la eLearning Afrika.
“ Tanzania inaendeleza dhamira yake ya mageuzi ya kidigitali katika elimu na tungependa kushirikiana na Serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na wanazuoni ili kufanya e- learning kuwezeshwa kwa ghrama nafuu kwa wote ,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa Tanzania imedhamiria kuongoza katika mageuzi ya kidigitali barani Afrika ambapo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inatambua kuwa mageuzi ya kidijitali ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi, maendeleo ya kijamii na ushindani wa kimataifa. Ili kufanikisha hili, Tanzania imeandaa mifumo kadhaa ikwemo Sera ya Taifa ya TEHAMA na Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali Tanzania 2024-2034.
Dkt. Biteko amesema kuwa Mkakati wa Taifa wa Elimu ya Kidijitali na Programu ya Tanzania ya Kidijitali zinalenga kuimarisha miundombinu na huduma za kidijitali, kuhakikisha teknolojia muhimu, vifaa, muunganiko na rasilimali za e-learning vinafika maeneo mbalimbali nchini, aidha nchi zingine pia zitumie rasilimali zao katika kusaidia mageuzi ya kidijitali katika nchi zao.
Amewahimiza wadau wa kongamano hilo kuwa ili mageuzi ya kidijitali ya Afrika yaweze kufanikiwa, lazima kuwezeshwa kwa nguvu kazi yenye ujuzi kuanzia umri mdogo. Tanzania imefanya marekebisho ya Sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo mwaka 2023 na kuwa ni mfano muhimu, ikisisitiza uendelezaji wa ujuzi kuanza elimu ya msingi.
“Sera hii pia inakuza matumizi ya teknolojia za kidijitali ili kukabiliana na upungufu wa walimu, kupanua upatikanaji wa elimu, na kuboresha ubora wa kujifunza. Mbinu hii inawaandaa wanafunzi kwa ajili ya baadaye na kuwawezesha waelimishaji kwa kuwapa zana bora za kufundishia katika nyakati za kidijitali,” amesema Dkt. Biteko.
Pamoja na hayo amesema kuwa Afrika lazima iendelee kuboresha mazingira kwa kampuni za kibunifu ya ndani kwa kuunda sera saidizi zinazokuza ubunifu na ujasiriamali ili kusaidia kukuza masoko ya ndani kwa teknolojia zinazoweza kuhamishwa na kuwezesha mataifa ya Afrika kuongeza ufanisi wa rasilimali, kupunguza ucheleweshaji na kuharakisha mageuzi ya kidijitali.
Pia amebainisha kuwa ni muhimu kwa Bara la Afrika kuwabakisha wataalamu wenye ujuzi ndani ya Afrika na kushirikisha diaspora ili kuchangia ukuaji wa bara hilo. Kwa kuifanya Afrika kuwa kitovu cha maendeleo ya kiteknolojia.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema Tanzania imeendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu kwa kuhamasisha matumizi ya akili mnemba katika shule.
Ameongeza kuwa kupitia Kongamano hilo lilianza Mei 7, 2025 litatoa fursa ya kuimarisha na kukuza uhusiano na ushirikiano katika nchi za Afrika sambamba na kuboresha sera na mifumo yake ya elimu ili kuendana na teknolojia, ubunifu na hususan matumizi ya akili mnemba.
Akieleza kuhusu eLearning Afrika, Mwanzilishi mwenza wa FIRCAD- Ghana, Dkt. Aida Opoku- Mensah amesema kuwa akili mnemba ina manufaa makubwa kwa maendeleo ya ikiwa ni pamoja na kutumika kutatua changamoto na kufanya shughuli kama binadamu.
Amesema akili mnemba imekuwa na umuhimu mkubwa katika maisha ya kila siku ya mwanadamu kwa kusaidia pia katika ufanyaji tafiti mbalimbali.
Amezungumzia utayari wa Afrika katika matumizi hayo na kusema kuwa baadhi ya nchi za Afrika zimekuwa na mwitikio wa haraka wa matumizi ya akili mnemba kuliko nyingine kutoka na uwekezaji wake.
Ametolea mfano Kenya (m-shule) na Nigeria tayari inatumia mifumo ya akili mnemba kwenye mifumo yake ya elimu na Tanzania kupitia ubongo kipindi kinachoelimisha na kuburudisha.
Amebainisha matumizi makubwa ya akili mnemba nchini China yamesaidia kukuza uchumi wake, aidha Afrika inatakiwa kuwekeza katika akili mnemba ili kusaidia katika sekta mbalimbali za elimu na miundombinu.
Kongamano na maonesho ya kila mwaka la eLearning Afrika , ambalo lilianzishwa mwaka 2005, ni tukio kubwa linalotoa fursa ya kubadilishana maarifa kwa elimu ya kidijitali, mafunzo na ujuzi katika Bara la Afrika.
Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mheshimiwa Salum Kalli, ameitembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Lekule mnamo Mei 7, 2025, ambapo alipata fursa ya kujionea maendeleo ya shule hiyo pamoja na kuzungumza na wanafunzi.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Kalli aliwahimiza wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuwa na nidhamu wawapo shuleni, akisisitiza kuwa elimu ndiyo njia pekee ya kufikia mafanikio ya maisha. Aliwataka kuepuka kabisa vitendo vya mimba za utotoni ambavyo vinaweza kuwa kikwazo kikubwa katika safari yao ya kielimu na kuwakatisha ndoto zao za baadae.
Aidha, kama sehemu ya kuwatia moyo, Mkuu huyo wa Wilaya aliwazawadia wanafunzi hao nyama ya ng’ombe kwa ajili ya chakula, jambo lililopokelewa kwa shangwe na furaha kubwa.
Akizungumza kwa niaba ya shule hiyo, Mkuu wa Shule Mwalimu Anna Wenseslausi alimshukuru sana Mkuu huyo wa Wilaya kwa ujio wake na zawadi aliyoitoa.
Na WAF, DODOMA
Serikali imesema huduma za afya ya akili zimeshajumuishwa kwenye vifurushi vya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), na hivyo wananchi wanaonufaika na bima wanaweza kupata matibabu hayo kwa mujibu wa mwongozo wa matibabu uliopo.
Akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Mhe. Jesca Msambatavangu, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa, huduma za afya ya akili, ushauri nasaha, pamoja na huduma za kibingwa kama vile utengamao, zote zimetajwa kama huduma muhimu kwenye Mwongozo wa Matibabu (Standard Treatment Guideline – STG) na zinagharamiwa na NHIF
“Huduma hizi zinalipiwa kwa kuzingatia aina ya dawa na ngazi ya kituo cha huduma, kwa mujibu wa mwongozo wa matibabu wa Taifa,” amefafanua Naibu Waziri Dkt. Mollel.
Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa huduma za afya ya akili zinapewa uzito sawa na huduma nyingine za msingi, na kuimarisha upatikanaji wake kupitia mifumo ya bima ya afya kwa wote.
Na John Mapepele
Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mhe. Mary Pius Chatanda ameshuhudia utiaji saini wa mikataba mitano ya bilioni 13.3 zilizotolewa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ili kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja wilayani Rufiji, huku Mhe. Mchengerwa akizindua rasmi Ligi ya ”Mchengerwa Mtu Kazi” inayoanza leo Mei 8, 2025 na kutoa vifaa (jezi na mipira) kwa timu zote 169 kutoka kwenye kata 13 zinazoshiriki mashindano hayo vyenye gharama ya milioni 67 pamoja na fedha taslimu milioni 25 ikiwa ni zawadi za washindi.
Tukio hili la utiaji saini limefanyika Mei 7, 2025 mara baada ya kukamilika kwa ziara ya siku mbili ya Mhe. Chatanda kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo, katika eneo la uwanja wa stendi wa Ikwiriri na kushuhudiwa na maelfu ya wananchi wa wilaya hiyo huku wasanii kadhaa wakitumbuiza kwa burudani za muziki.
Akitoa taarifa ya miradi hiyo, Meneja wa Wakala za Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Pwani, Leopold Runji amefafanua kuwa gharama hizo zinahusisha ukarabati wa barabara ya Nyamwage yenye Kilomita 28, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Chumbi- Kiegele yenye kilomita 1.4, ukarabati wa barabara ya Mohoro- Mtanga kilomita 12.3 na Mohoro Ndundutawa yenye kilomita 7.5.
Pia ukarabati wa barabara ya Nyamwage- Mpakani- Nambunju na ujenzi wa barabara za lami katikati ya mji wa Ikwiriri ambapo amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kuiunganisha wilaya hiyo na maeneo mbalimbali ya mikoa ya Tanzania.
Mhe. Chatanda amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za miradi na kufafanua kwamba kwa kufanya hivyo siyo tu ametekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa mafanikio makubwa bali ameleta mapinduzi katika sekta ya miundombinu kote nchini.
Amempongeza Mhe. Mchengerwa kwa kusimamia utekelezaji wa miradi yote kwa kiwango cha juu huku akitoa wito kwa maeneo mengine nchini kuiga utekelezaji huo.
”Ndugu zangu hapa ni vema tuwe wakweli, unaweza ukaletewa fedha za maendeleo lakini ukashindwa kutekeleza lakini,hivyo nampongeza mbunge wenu kwa kusimamia utekelezaji wa miradi hii ambayo inakwenda kuleta tija kubwa kwa wananchi katika Wilaya ya Rufiji” amefafanua Mhe. Chatanda
Mbali na kukagua miradi ya Serikali pia ameshuhudia ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa chama, pia ameshuhudia mradi mkubwa wa ujenzi wa ukumbi wa kisasa wa wilaya unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 2.5 unaofadhiliwa na Mbunge wa Rufiji Mhe. Mchengerwa kwa kupitia marafiki na wadau mbalimbali.
Akizungumzia kuhusu miradi ya elimu katika wilaya hiyo, Mhe. Chatanda amesema amefurahishwa na kazi nzuri ya ongezeko kubwa la Shule za Msingi na Sekondari na kutoa wito kwa wananchi kuwapeleka watoto wao katika shule hizo ili kuunga mkono maono ya Mhe. Rais ya kuwakomboa wananchi kielimu pia kwa manufaa makubwa ya taifa na vizazi vyao.
Mbunge wa Rufiji Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa Serikali imefanya kazi kubwa ya ujenzi wa shule ambapo amesema wakati anaingia kwenye ubunge kulikuwa na na Shule za Msingi 40 tu ambapo sasa kuna shule 63 na upande wa Vituo vya Afya, awali kulikuwa na vituo 3 na sasa vimefika 9, huku asimshukuru Mhe. Rais Samia kwa maono makubwa ya kuwaletea maendeleo watanzania.
Aidha, Mhe. Chatanda alipotembelea na kukagua ukarabati wa hospitali ya Wilaya ya Rufiji na ujenzi wa kichomea taka katika eneo la Utete uliogharimu takribani milioni 900 na kuwataka wananchi kutumia huduma hizo ikiwa ni pamoja na wanaume kuwa msitari wa mbele kuwapeleka wake zao kwenye huduma za kliniki ili kujua afya za wenza wao na watoto.
Akizungungumzia kuhusu ukatili wa kijinsia, amewataka wazazi kuwalea watoto wao katika misingi maadili ili waweze kuja kuwa wazazi bora badala ya kuwaacha kujifunza kwenye mitandao.
Wakati huo huo ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kupiga kura huku akisisitiza kuchagua CCM kwa kuwa ndicho chama kilichowaletea maendeleo.