Na Joachim Nyambo.Mbeya.


WITO umetolewa kwa wajawazito na wanawake wanaonyonyesha kuchukua tahadhari juu ya matumizi ya dawa zilizo na kemikali aina ya zebaki kutokana na kemikali hiyo kuhatarisha afya za watoto waliopo tumboni ikiwemo kuathiri ukuaji wa ubongo.


Miongoni mwa dawa zinazotwajwa kuwa na kemikali hizo hatarishi kwa watoto waliopo tumboni na wachanga ni pamoja na dawa aina ya Dental Amalgam itumikayo kuziba meno yaliyotoboka iliyo na asilimia hamsini ya zebaki.


Afisa Programu wa Asasi isiyo ya kiserikali ya Agenda,Dorah Swai alibainisha hayo wakati wa mafunzo kwa wataalamu wa afya ya kinywa na meno yaliyofanyika jijini Mbeya kwa ushirikiano wa  Wizara ya Afya na asasi hiyo.


Kutolewa kwa mafunzo hayo ni sehemu ya Mpango wa kuhamasisha  upunguzaji wa matumizi ya dawa iliyo na zebaki itumikayo kuziba meno yaliyotoboka ikiwa ni utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wenye lengo la  kulinda afya na mazingira kutokana na athari za Zebaki wa Minamata wa Zebaki wa Mwaka 2013.


Swai alisema Zebaki ina athari kubwa kwa afya na mazingira ikiwemo kuharibu ukuaji wa ubongo wa motto tangu akiwa tumboni mwa mama ambapo kemikali hiyo inaweza kutoka kwa mjamzito na kuingia kwa mtoto wakati wa ujauzito huo.


Alisema pia upo uwezekano wa Zekani kuhama kwa mama kwenda kwa mtoto kupitia maziwa ya mama wakati wa kunyonyesha na hivyo kuendelea kuhatarisha afya ya mtoto husika hata baada ya mama kujifungua iwapo ataendelea kutumia dawa zilizo na kemikali hizo.


Afisa huyo alitaja matokeo ya kuathiriwa kwa ukuaji sahihi kwa ubongo wa mtoto tangu angali mchanga kuwa ni pamoja na kuharibu  uwezo wa mtoto husika wa kufikiri na hatimaye kumfanya ashindwe kushiriki kikamilifu kwenye kuchangia maendeleo ya taifa lake hapo baadaye.


“Kutokana na athari hizi ni muhimu jamii na wataalamu wa afya wakijizatiti kuwalinda wanawake wajawazito na wanaonyonyesha.Tutumie dawa zilizo sahihi kwa ustawi wa jamii yetu ili kuendelea kuwa na Tifa lililo na watu wenye maamuzi sahihi na wenye mchango katika kila Nyanja ya kijamii.” Alisema.


Kwa upande wake Mratibu wa Afya ya Kinywa na Meno wa Wizara ya Afya,Dkt Baraka Nzobo alisema wajawazito na wanawake walio katika umri wa kuzaa wako hatarini zaidi iwapo watatumia dawa au vyakula vilivyo na Zebaki.


Dkt. Nzobo alisema kwa sasa ni kazi ya wataalamu kuunga mkono juhudi za serikali na wadau mbalimbali nchini katika kutekeleza mwongozo wa Mkataba wa Minamata kwakuwa  za kuziba meno zisizo na  Zebaki zinapatikana kwa wingi nchini.


Mmoja wa wataalamu wa Afya ya Kinywa na Meno katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya(MZRH),Omary Matola alisema kutolewa kwa mafunzo hayo kunaendelea kutoa mwanya wa uelewa kwa watoa huduma ya meno juu ya athari za Zebaki naa kuweka msisitizo wa kuifanya jamii kuwa salama.


Baadhi ya wagonjwa waliokutwa wakisubiri huduma katika Hospitali ya MZRH walikiri kutokuwa na uelewa juu ya athari zitokanazo na kemikali za iana yoyote bali wanachozingatia wao ni kupata huduma waliyoifuata baada ya kusumbuliwa na matatizo ya meno.


“Ndugu yangu sisi tunafuata tunachoambiwa na wataalamu tukija hapa.Ni ngumu sana ukiwa na shida uanze kuhoji.Hivi si unajua jino likikubana kaka.Mimi mwenyewe nakuambia leo hatujalala..huyu ndugu yangu kalia usiku kucha ..nini?..jino.?Unadhani utafikiria na kuuliza hayo mambo.Alisema Mkazi wa Mama John jijini Mbeya aliyesema amemsindikiza dada yake kwaajili ya kupata huduma hospitalini hapo.”

Mwisho.
Mtaalamu Afya ya Kinywa na Meno katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya(MZRH),Omary Matola akionesha kwa wanahabari dawa zinazotumika katika matumizi ya ktibu meno yaliyotoboka kwa kuyaziba wakati walipotembelea chumba cha kutolea huduma hiyo.(Picha na Joachim Nyambo)

Share To:

JUSLINE

Post A Comment: