Na Joachim Nyambo.


USHIRIKIANO kati ya Muungano wa Klabu za waandishi wa habari nchini(UTPC) na Sida umeendelea kuimarika ambapo jana katika ofisi za UTPC, Balozi wa Sweden nchini Tanzania Bw. Anders Sjoberg alitia saini makubaliano ya kuendelea kuifadhili UTPC kwa mwaka mwingine mmoja wakati majadiliano ya kuufadhili Mpango Mkakati mpya wa UTPC yakiendelea.


Katika hotuba yake mara baada ya kutia saini mkataba huo, Balozi Sjoberg alisema ameridhishwa sana na namna UTPC inavyozilea klabu za waandishi wa habari hasa kwa kuwa amepata wasaa wa kutembelea klabu nyingi nchini na amejionea klabu zinavyojiamini kutekeleza majukumu yake ya kihabari.


Akizungumzia swala la demokrasia, uhuru wa kujieleza na uhuru wa habari, Balozi Sjoberg alisema Sweden inaamini kuhusu demokrasia, haki, uhuru wa kujieleza na uhuru wa habari hivyo basi itaendelea kuifadhili UTPC ili iendelee kuimarika zaidi na kusimamia uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza nchini.


Katika hotuba yake, Mkurugenzi wa UTPC,Aboubakar Khasan alishukuru Sida kwa kuendelea kuiamini taasisi ya UTPC na kwamba UTPC itaendelea kuzisimamia klabu za waandishi wa habari kwa ubora zaidi kufikia malengo ambayo wamejiwekea lakini pia kushawishi na kutetea uhuru wa habari nchini na upatikanaji wa maslahi bora ya mwandishi wa habari.


Naye Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Mwanza Bw. Edwin Soko, aliomba Sida kuipa kupaumbele taasisi ya UTPC kwa kuwa inafanya kazi kubwa ya kusimamia klabu za waandishi wa habari ambazo zimebeba idadi kubwa ya waandishi wa habari nchini.


Hata hivyo aliiomba Sida kuanza kufikiria namna ya kuisaidia tasnia ya habari kwenye masuala ya ulinzi na usalama wa mwandishi wa habari hasa tunapoeleka kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.


Akitoa shukrani kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Bi. Paulina David aliwashukuru Sida kwa kuendelea kuisaidia UTPC lakini pia alisisitiza kwamba kupitia Bodi ya Wakurugenzi fedha hizo zitasimamiwa vizuri.


 

Balozi wa Sweden nchini Tanzania Bw. Anders Sjoberg(kushoto) na na mwenyeji wake,Mkurugenzi wa UTPC,Aboubakar Khasan wakitiliana saini makubaliano ya Sida kuendelea kuifadhili UTPC kwa mwaka mwingine mmoja wakati majadiliano ya kuufadhili Mpango Mkakati mpya wa muungano hu yakiendelea.(Picha na UTPC)

Share To:

JUSLINE

Post A Comment: