Wafugaji Jamii ya Wamasai wakiwa kwenye mkutano wa kujadili htima yao wilayani Ngorongoro mkoani Arusha jana. 


Na Mwandishi Wetu, Arusha 


WAFUGAJI wa jamii ya wamasai wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wamesema kamwe hawajawahi na hawatafanya hivyo kuwazuia watu wanaoishi eneo la Ngorongoro wanaotaka kuhama kwa hiari yao wenyewe kwani wanaofanya hivyo ni uhuru wao. 

Aidha, wamesema serikali nayo kwa upande wao isimlazimishe mtu yeyote kuondoka eneo la Ngorongoro hasa kutokana na baadhi ya watu wakiwamo wabunge kutaka majeshi yatumike kuwaondoa. 

Walisema hayo juzi (Machi 13) katika mkutano wa wafugaji wa tarafa ya Ngorongoro uliofanyika jijini Arusha kujadili hatma yao kuhusiana na mgogoro unaoendelea ambapo serikali inataka wafugaji wanaoishi ndani ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuondoka ili kupisha uhifadhi. 

Joseph Ole Shangay akizungumza wakati wa mkutano huo alisema serikali isiweke mazingira yeyote ya kumlazimisha mtu aondoke bila ridhaa yake kwani kufanya hivyo itakuwa ni kukiuka haki za binadamu. 

"Baadhi ya watu wanasema waondoke sababu ni maskini, kama kweli kumuondoa mtu eneo kwasbabu tu ni maskini basi hii nchi tuhame maana inaogelea kwenye umaskini," alisema. 

Ole Shangay ambaye pia ni wakili alisema kinachofanywa na serikali ni sawa na fisi akitaka kuwala watoto wake anawayengeneza wawe na halufu kama ya mbuzi ili apate sababu ya kuwaua na kuwala 

Kuhusu idadi ya mifugo, alisema kwamujibu wa ripoti iliyofanyika 2017 ilionesha kuwa Ngorongoro kuna mifugo 230,000 ambayo ni sawa na ongezeko la takribani mifugo 20,000 toka mwaka 1959 ambalo ni ongezeko dogo sana. 

Oleshangay alisema kimsingi wafugaji halisi wa eneo la Ngorongoro hawana mpango wa kuhama eneo hilo na kuiomba serikali isitishe mchakato wake wa kutaka kuwaondoa kwababu wapo Ngorongoro kisheria na sio kama wavamizi. 

Aidha, alisema jamii ya wamasai hawana mahusiano yeyote ya kiimani wala ya kihistoria na eneo linaloitwa Malya ambako hivi karibuni kulifanyila mkutano na viongozi wa serikali kuhudhuria. 

Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro, Edward Maura, alisema inashangaza kuona serikali inakazana na mipango ya kutaka kuwaondoa wenyeji wa Ngorongoro kwa madai kuwa hidadhi ya Ngorongoro ipo hatarini kupotea kitua ambacho hakina ukweli. 

"Watanzania na dunia nzima puuzeni taarifa ya kwamba watu wa Ngorongoro wamekubali kuhama kwa hiari yao, puuzeni hiyo sio habari, hatuna mpango wala mkakati wa kukubaliana na mtu yeyote kuondoka eneo la Ngorongoro," alisema. 

Maura alisema Ngorongoro ina mfumo rasmi wa uongozi wakiwamo malaigwanan, wenyeviti wa vijivini, madiwani na mbunge hawakuhudhuria mkutano wa hivi karibuni ulioitishwa na Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa, uliofanyika jijini Arusha. 

Alisema hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikipata sifa kimataifa na kuongezeka kwa mapato kila mwaka hivyo sababu ya kwamba hifadhi ipo hataririni kupotea kutokana na watu na mifugo wanaoishi ndani  haina msingi propaganda hiyo inafanywa kwa maslahi ya watu wachache wenye maslahi yao binafsi. 

Kwa upande wake kiongozi wa Malaigwanani Ngorongoro, Metui OleShaudo, alisema inasikitisha baadhi ya viongozi kuwaita wananchi wa Ngorongoro kwamba ni raia wa Sudani na kwamba sio raia wa Tanzania wakati sio kweli wao ni Watanzania halali wa kuzaliwa. 

"Endapo sisi ni wasudani basi tusipelekwe Handeni aje rais wa Sudani tuzungumze naye hapa na tuhamishiwe twende Sudan," alisema. 

Oleshaudo alisema wako tayari kukaa na serikali kuzungumza namna ya kuendeleza uhifadhi katika hifadhi ya Ngorongoro lakini sio suala la kuhama eneo la Ngorongoro. 

Naye Lazaro Saitoti alisema inashangaza kuona mikakati ikiendelea kupangwa kutaka kuwaondoa eneo la Ngorongoro wakati kimsingi hakuna ushahidi wowote unaonyesha kuwa wafugaji wanaoishi eneo hilo wanahatarisha maisha ya wanyamapori. 

"Tunahitaji serikali ije na 'fact' je kwa muda wote ambao tumekuwa Ngorongoro  toka tulipotoka Serengeti ni ngo'mbe gani amekula Simba, ni mbuzi gani amekula chui au pundamilia maana ndo mifugo ambao tunaishi nao kwa muda wote na hakuna mnyamapori aliyeuawawa na mifugo yetu,alisema. 

Diwani wa Kata ya Endulen,James Moringe, amemuomba rais Samia Suluhu Hassan kuruhusu miradi ya maendeleo iliyosimamishwa tarafa ya Ngorongoro iendelee kujengwa kwasababu kuisimamisha kunawathiri wananchi.

 Moringe alisema katika kikao walichofanya na Waziri Mkuu Februari 17, mwaka huu wafugaji walieleza hujuma mbalimbali dhidi ya wanyamapori zinazofanyika ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kwa wahusika ambao ni watumishi ndani ya hifadhi hiyo. 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: