Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi(Mb) amewaonya wananchi waliong'oa mabango yaliyowekwa na kuharibu alama za mipaka kwa ajili ya utunzaji wa chanzo cha maji katika vijiji vya Chiwachiwa na Kisegese Wilaya ya Kilombero Mkoa wa Morogoro.


Mahundi ametoa onyo hilo katika mwendelezo wa ziara yake mkoani Morogoro ambapo amesikitishwa na watu wasiojullikana kuharibu miundombinu ya mradi huo unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni tatu.


Amesema serikali kupitia Rais Samia Siluhu Hassan imeelekeza fedha nyingi kwenye miradi ya maji na kwamba Wizara haitavumilia uharibifu unaofanywa na tayari uchunguzi umeanza watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.


Eneo hilo la mto Lwipa lipo chini ya usimamizi wa bodi ya maji bonde la mto Rufiji ambao waliweka bikon mia mbili kuzunguka eneo hilo ikiwa ni ishara ya ukomo wa shughuli za kibinadamu lakini kundi la watu wasiofahamika wameng'oa bikoni mia moja themanini.


Amewataka wananchi kuilinda miundo mbinu ya maji kwani serikali inatumia fedha nyingi ili kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.


Kwa upande wake meneja wa Wakala wa maji vijijini RUWASA Wilaya ya Kilombero Flolence Mlelwa amesema kwa sasa serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa tanki la lita laki mbili na nusu na mradi unatarajiwa kuhudumia vijiji vyote Kata ya Mbingu na Igima ambapo vituo thelathini vikitarajiwa kujengwa.


Mhandisi Aron Kilamba mkandarasi wa tanki la maji ameiomba jamii kuwa sehemu ya utekelezaji na walinzi wa mradi.


Mbunge wa Jimbo la Mlimba Godfrey Kunambi ameishukuru serikali kwa kutatua changamoto iliyokuwa inawakabili wananchi wake ya upatikanaji wa maji safi na salama Jimboni kwake.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: