Na Joachim Nyambo,Mbarali. 


MWAMKO wa ujenzi wa vyoo bora umetajwa kuzidi kuimarika kadiri elimu na hamasa inavyoendelea kutolewa wilayani Mbarali mkoani Mbeya na kuanza kuwaepusha wananchi kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu ambacho awali kilikuwa kikiwasumbua.


Uchunguzi unaonesha kuwa awali wakazi wengi wilayani hapa walikuwa na mwamko mdogo wa kuwa na vyoo hatua iliyowalazimu baadhi yao kujisaidia vichakani na kuhatarisha afya zao na majirani.


Watoto wadogo hususani wanaotambaa walikuwa hatarini zaidi kupata magonjwa ya kuhara hasa kwa wale waliokosa uangalizi wa karibu waliookota vitu mbalimbali ikiwemo udongo na kuvipeleka mdomoni wakijua ni sehemu ya vyakula.


Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo,Dk Godfray Mwakalila alibainisha hayo alipozungumza na Mtandao huo katika maadhimisho ya siku ya Choo duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Novemba 19 ya kila mwaka.


Kwa mujibu wa Dk Mwakalila katika miaka ya nyuma hata wakazi waliokuwa na vyoo waliokuwa navyo kama ushahidi ttu wa kuonesha kaya husika ina choo lakini kwa uhalisia katika nadharia ya ubora havikuwa vyoo bora.


Alisema kutokana na kuwa na kukosekana kwa vyoo vituo vya utoaji huduma za matibabu vilijikuta vikipokea wagonjwa wengi wakiwemo watoto wadogo hasa walio na umri wa kutambaa waliougua magonjwa ya kuhara.


Pamoja na hatua iliyofikiwa kwa sasa daktari huyo anasema bado bado wilaya hiyo iko nyuma katika ujenzi wa vyoo vya kisasa licha ya kuwa kwenye ujenzi wa vyoo vya kawaida imepiga hatua.


Miongoni mwa wakazi waliopewa mkazo wa kujenga vyoo bora ni pamoja na waishio katika Mamlaka ya mji mdogo wa Rujewa yalipo makao makuu ya wilaya. 


Mwakalila alisema kama wilaya nguvu kubwa inawekezwa kwa sasa kutoa elimu ya ujenzi wa vyoo bora kwa wananchi badala ya kuendelea kujenga kwa mazoea ili mradi kaya husika ionekane kuwa ina choo. 


Alisema licha ya mwamko unaoonekana kwa sasa kama viongozi wangetamani kuona wakazi wanapiga hatua zaidi na kujenga vyoo vya kisasa vilivyo bora na vyenye muonekana wenye kuendana na nyumba zao za kisasa wanazojenga. 


Akizungumzia hali hiyo,Mkuu wa wilaya ya        Mbarali,Reuben Mfune alikiri asilimia za ujenzi wa vyoo bora wilayani hapa kuwa chini na kuongeza kuwa jitihada za makusudi zinahitajika kuelimisha wananchi. 


“Wananchi ni muhimu wakaelewa kuwa kwa tulipofikia kwa sasa hatuzungumzii kuwa tu na vyoo bali tuwe na vyoo bora.Na hili viongozi wa mitaa,vitongoji wanapaswa kulifuatilia kwa karibu kuwapa elimu na mifano wananchi wao.”alisema Mfune.


Changamoto ya kujisaidia hovyo wilayani hapa inatajwa pia kuwemo katika maeneo zinakofanyika shughuli za kilimo hususani cha zao la mpunga ambapo wakati wa msimu wa kilimo wakulima na vibarua wao hupiga kambi mashambani lakini asilimia yao kubwa hawana vyoo na hijusaidia vichakani na kwenye mifereji ya maji wanayotumia kumwagilia mashamba.


Dk Mwakalila anaitaja hatua hii kuwa sehemu ya mambo yanayohatarisha afya za watu wote wanaokuwa kwenye maeneo hayo wakiwemo watoto wadogo ambao wazazi wao hutumia maji hayohayo kwa matumizi ya kawaida ikiwemo kunywa,kupikia na hata kuwaogesha watoto wadogo ambao kwa uchjanga wao bado ngozi na matumbo yao haviwezi kuhimiri wanapokutana na vijidudu vya magonjwa.


“Maeneo yote yanayolimwa mpunga kumekuwa na matukio mengi ya ugonjwa wa kichocho.Inamaanisha watu wanakunywa maji yaliyokojolewa.Lakini pia maji wanayokunywa yanakuwa yameungana nay ale yaliyokaa kwenye madimbwi kwa muda mrefu hivyo ni hatari zaidi.”


“Tunahitaji kuchukua tahadhari ili kulinda afya zetu.Sote tunatambua pia kwenye mashamba yetu ya mpunga hakuna vyoo kule hivyo watu wanajisaidia hovyo sasa kwa kipindi kama hiki ambacho maji husambaa mashambani inakuwa rahisi kusambaza magonjwa.Tunashauri unapotoka nyumbani beba dumu lenye maji safi na salama uliyochemsha ndiyo utumie unapopata kiu shambani.”alisisitiza.


Aliyasema haya alipozungumza na wenyeviti wa mitaa katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Rujewa na kuwataka wafanye mikutano kwenye maeneo yao ili kutoa elimu hiyo.


Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Rujewa,Chameta Godigodi pamoja na kukiri mwenendo wa maisha ya wakulima wa mpunga kutotofautiana na yaliyosemwa na daktari aliwasihi wenyeviti wenzie kuwahimiza wananchi kutambua kuwa kinga ni bora kuliko tiba.


Godigodi alisema kwa kuchukua tahadhari ya kubeba maji safi na salama kwaajili ya kunywa wakiwa shambani sit u kutaipunguzia Serikali gharama za kuwatibu bali pia kutawapunguzia adha ya kutumia muda wao kwenda kufuata matibabu badala ya kufanya kazi za kujiingizia kipato. 


“Ndugu zangu kama ushauri tumeupata na kwetu sisi haya ni maelekezo tunatakiwa kwenda kuyatekeleza kwa kuwashauri watu wetu.Ni muhimu wakulima wetu na wananchi kwa ujumla wakatambua kuwa hakuna haja ya kusubiri uugue uanze kupoteza muda kwenda hospitali na kugharamia matibabu.Tufuate ushauri wa kuchukua tahadhari ili tusifike huko.”alisisitiza Godigodi.

Share To:

Post A Comment: