Asteria Muhozya na Abubakari W Kafumba


Tanzania imekutana na Kampuni ya CMA CGM inayojishughulisha na masuala ya usafirishaji wa mazigo yenye Makao Makuu yake Dubai ikiwakilishwa na Mkurugenzi wa Biashara wa kampuni hiyo kwa upande wa Afrika Gulliaume Adam. Gulliaume ametaka kujua kuhusu maendeleo ya sekta ya madini na kueleza nia ya kampuni hiyo kusafirisha madini kutoka Tanzania.


Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini Bw. Venance Kasiki amemweleza mwakilishi huyo pia kuhusu uwepo wa fursa nyingine mbali na ya kusafirisha madini ambazo kampuni hiyo inaweza kuzitumia ikiwemo kuwekeza katika shughuli za uchimbaji na ununuzi wa madini.


‘’Sio tu biashara ya kusafirisha kuna fursa nyingi kwenye sekta ya madini nchini fikirieni pia kuhusu kuchimba, kununua ama kusafirisha mizigo kwenye migodi. Msisite kuitumia Tume ya Madini kupata taarifa zaidi kuhusu masuala haya. Serikali ipo karibu sana na wawekezaji kwa hiyo msihofu kuhusu upotevu wa fedha wala udanganyifu,’’ amesema Kasiki.


Aidha, Kamishna Jenerali wa banda la Tanzania kwenye maonesho hayo Balozi Mohamed Mtonga, baada ya kupata mrejesho wa Sekta ya Madini amezitaka sekta muhimu kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa nchini kuchangamkia fursa kupitia maonesho hayo. ‘’Fursa hii ikipita imepita, tuitumie vizuri nafasi hii kuwaeleza tulivyonavyo nchini kwetu ili waje kushirikiana nasi. Karibia dunia yote iko hapa na sisi tuna bahati kwamba hatuko nyuma,’’ amesisitiza balozi Mtonga.

Hatua hiyo inafungua fursa ya uwekezaji katika uchimbaji baina ya Tanzania na wawekezaji kutoka nje ya Tanzania. 

Share To:

Post A Comment: