Friday, 5 November 2021

SERIKALI KUZIDI KUONDOA TOZO ZINAZOKWAMISHA MAENDELEO SEKTA YA UVUVI

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah akiwa ameshika samaki aina ya sangara baada ya kufika katika Mwalo wa Ihale uliopo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu na kuzungumza na wavuvi juu ya dhamira ya serikali ya kuondoa na kurekebisha tozo za uvuvi ambazo siyo rafiki kwa wadau wa uvuvi pamoja na kukagua ujenzi wa sehemu ya kushushia samaki, kuhifadhia, kuuzia pamoja na ofisi ya Kikundi cha Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU). (Picha na Edward Kondela – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) akipewa maelezo na Afisa Uvuvi Mkuu kutoka katika wizara hiyo Bw. Melkizedeck Koddy (kulia) juu ya ujenzi wa Mwalo wa Ihale uliopo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu unaojumuisha sehemu ya kushushia samaki, kuhifadhia, kuuzia pamoja na ofisi ya Kikundi cha Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU). Anayefuatilia maelezo hayo (katikati) ni Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. George Kwandu. (Picha na Edward Kondela – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah (aliyevaa miwani) akikagua ujenzi wa sehemu ya kuhifadhia na kuuzia samaki pamoja na ofisi za Kikundi cha Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) Mwalo wa Ihale, uliopo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu ambapo amemtaka mkandarasi kukamilisha ujenzi huo Tarehe 30 Mwezi Novemba Mwaka 2021. Anayemuongoza Dkt. Tamatamah ni Mwenyekiti wa BMU Mwalo wa Ihale Bw. pius Mazima. (Picha na Edward Kondela – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah (wa tatu kushoto) akikagua ujenzi wa jengo la ofisi ya Kituo cha Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP) Kanda ya Simiyu na Magu lililopo Kasadima Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu akiwa na baadhi ya maafisa kutoka wizarani na Wilaya ya Busega na kutoa maelekezo kwa mkadarasi kukamilisha ujenzi wa jengo hilo ifikapo Tarehe 30 Mwezi Novemba Mwaka 2021. (Picha na Edward Kondela – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Muonekano wa maendeleo ya ujenzi wa sehemu ya kushushia samaki, kuhifadhia, kuuzia pamoja na ofisi ya Kikundi cha Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) Mwalo wa Ihale uliopo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu, ambapo ujenzi huo unakadiriwa kufikia zaidi ya asimilia 50 ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu Shilingi Milioni 162. (Picha na Edward Kondela – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

 

Muonekano wa maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP) Kanda ya Simiyu na Magu kilichopo Kasadima Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu ambapo ujenzi huo unakadiriwa kufikia asimilia 80 ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu Shilingi Milioni 285. (Picha na Edward Kondela – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Mkuu wa Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu Mhe. Gabriel Zacharia akimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah, wakati katibu mkuu huyo alipofika katika ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo, kwa ajili ya kutoa maelezo ya ufupi juu ya miradi mbalimbali ambayo Wizara ya mifugo na Uvuvi inatekeleza nchini, ikiwemo iliyopo katika Wilaya ya Busega ya ujenzi wa sehemu ya kushushia samaki, kuhifadhia, kuuzia pamoja na ofisi ya Kikundi cha Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) Mwalo wa Ihale na ujenzi wa Kituo cha Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP) Kanda ya Simiyu na Magu. (Picha na Edward Kondela – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)


Na. Edward Kondela

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema tozo nyingi katika sekta ya uvuvi ambazo zipo chini ya wizara tayari zimeboreshwa na nyingine kuondolewa ili kuweka mazingira mazuri zaidi ya kufanya kazi kwa wadau wa uvuvi nchini.

 

Dkt. Tamatamah amesema hayo (04.11.2021) katika Mwalo wa Ihale uliopo Wilaya ya Busega, Mkoani Simiyu, wakati akikagua ujenzi wa sehemu ya kushushia samaki, kuhifadhia, kuuzia pamoja na ofisi ya Kikundi cha Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika mwalo huo, ambapo amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wizara zingine pamoja na halmashauri za wilaya kote nchini zinaendelea kuangalia tozo za uvuvi ambazo siyo rafiki kwa wadau wa uvuvi.

 

Amesema nia ya serikali ni kuondoa vikwazo vya biashara na utekelezaji wa agizo kutoka katika mamlaka ya juu ya serikali katika mwaka huu wa fedha 2021/22 wa kuondoa tozo ambazo zinakwamisha maendeleoa ya sekta mbalimbali nchini.

 

“Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama yetu Samia Suluhu Hassan alisema katika wizara zote ziangalie upya tozo ambazo katika ile sekta zipo kwa kushirikiana na halmashauri kwa mfano sisi wizara ambazo zipo chini ya wizara nyingi tumezipunguza, kila tunapopita katika halmashauri tunawaambia pamoja na wizara zingine juu ya tozo zinazohusu sekta ya uvuvi.” Amesema Dkt. Tamatamah

 

Katibu mkuu huyo amebainisha hayo baada ya kukutana na baadhi ya wadau wa uvuvi katika Mwalo wa Ihale na kujulishwa juu ya tozo mbalimbali za sekta ya uvuvi ambazo wanaona zimekuwa zikiwakwamisha kufanya biashara.

 

 

Awali akiwa katika ofisi ya Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amekutana na mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Gabriel Zacharia ambaye pia alimfahamisha Dkt. Tamatamah juu ya uwepo wa tozo ambazo wadau wa uvuvi wamekuwa wakizilalamikia ikiwemo ambayo inatozwa kwa thamani ya dola za kimarekani.

 

Aidha, Mhe. Zacharia ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kubainisha kuwa kumekuwa hakuna malalamiko makubwa kutoka kwa wadau wa uvuvi juu ya mambo mengine ambayo sekta ya uvuvi inahusishwa ukizingatia Wilaya ya Busega ndiyo wilaya pekee katika Mkoa wa Simiyu ambayo ina sehemu ya Ziwa Victoria.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah akiwa kwenye ukaguzi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Kituo cha Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP) Kanda ya Simiyu na Magu lililopo Kasadima na ujenzi wa Mwalo wa Ihale katika ya Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu, amesema ameridhishwa na ujenzi unavyoendelea huku akiwataka makandarasi kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo ifikapo Tarehe 30 Mwezi Novemba Mwaka 2021, ambapo Mwenyekiti wa Kikundi cha Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) Mwalo wa Ihale Bw. Pius Mazima amesema mradi uliopo katika mwalo huo utakuwa na tija kwao na watahakikisha wanautumia vizuri.

 

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema nia ya serikali ni kuhakikisha mialo yote nchini inakuwa na mitambo ya kuzalisha barafu ili wavuvi wapate barafu kwa bei nafuu kwa ajili ya kuhifadhia samaki.

 

Kwa mujibu wa taarifa za miradi aliyotembelea Katibu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah katika Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu, ujenzi wa sehemu ya kushushia samaki, kuhifadhia, kuuzia pamoja na ofisi ya Kikundi cha Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) Mwalo wa Ihale unakadiriwa kufikia zaidi ya asimilia 50 ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu Shilingi Milioni 162 na ujenzi wa Kituo cha Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP) Kanda ya Simiyu na Magu unakadiriwa kufikia asimilia 80 ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu Shilingi Milioni 285.

 

Mwisho.

No comments:

Post a Comment