Thursday, 11 November 2021

MTENDAJI MKUU TARURA AMTAKA MKANDARASI KUONGEZA JUHUDI UJENZI WA BARABARA ZA LAMI MJI WA SERIKALI

 MTENDAJI MKUU TARURA AMTAKA MKANDARASI KUONGEZA JUHUDI UJENZI WA BARABARA ZA LAMI MJI WA SERIKALI


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor H. Seff amemtaka Mkandarasi Kampuni ya China Heinan International Cooperation Co. Ltd (CHICO) anayetekeleza mradi wa ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa Km 51.2 katika Mji wa Serikali Mtumba kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo kwa muda uliopangwa ifikapo tarehe 31 Desemba, 2021.

Mhandisi Seff ameyasema hayo leo tarehe 11 Novemba, 2021 wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma kwa lengo la kuangalia maendeleo ya kazi zilizobakia na kumsisitiza Mkandarasi kuongeza juhudi kwakuwa hakutakuwa na muda wa nyongeza wa kukamilisha kazi hiyo.

“Namsisitiza Mkandarasi aongeze juhudi katika kukamilisha kazi hii kwasababu hakutakuwepo tena na muda wa nyongeza vinginevyo tutafuata vipengele vilivyopo katika mkataba ili kama atachelewa kukamilisha kazi kwa wakati atapata adhabu kama ilivyoainishwa kwenye mkataba”, amesema Mhandisi Seff.

Mhandisi Seff ameongeza kuwa maendeleo ya mradi ni mazuri yamefikia zaidi ya asilimia 80 na anategemea kwamba ifikapo tarehe 31 Desemba, 2021 kazi zote kubwa zitakuwa zimekamilika, kazi ya kuweka lami imebakia kama Km 2.1 na anatarajia kuwa sehemu hiyo ndogo iliyobakia itakamilika kabla ya mwezi Novemba kuisha.

Pia, Mtendaji Mkuu ameelezea changamoto ambayo ameiona ni kuhusu suala la maji ya mvua ambapo tayari changamoto hiyo imeanza kufanyiwa kazi ili kuzuia athari ambazo wananchi watapata wakati mvua zitakapoanza kunyesha kwani kazi hiyo ni muhimu na inatakiwa ifanyike ili kuokoa madhara ambayo yanaweza kuletwa wakati wa mvua.


Mradi wa ujenzi wa Barabara za Mji wa Serikali Mtumba unasimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na unatekelezwa na Mkandarasi China Heinan International Cooperation Co. Ltd (CHICO) ambapo utakamilika ifikapo tarehe 31 Desemba, 2021.


No comments:

Post a Comment