Mkuu wa Wilaya ya Hanang'  Janeth Mayanja, akikagua gwaride  wakati akifunga mafunzo ya Jeshi la Akiba katika hafla iliyofanyika Viwanja vya Kata ya Nangwa wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang'  Janeth Mayanja, akihutubia vijana waliohitimu mafunzo hayo.


Na Dotto Mwaibale, Hanang'


MKUU wa Wilaya ya Hanang' Janeth Mayanja amefunga Mafunzo ya Askari wa Jeshi la Akiba kwa Mwaka 2021  yaliyofanyika  Kata ya Nangwa wilayani humo.

Jumla ya wahitimu 83 wamemaliza na kufuzu Mafunzo hayo ya Jeshi la akiba kikamilifu sanjari mafunzo ya udereva  kutoka Chuo cha Nangwa VTC  na kukabidhiwa vyeti na mkuu wa wilaya hiyo Janeth Mayanja ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Mayanja amevishukuru vyombo vya ulinzi na usalama vilivyowaandaa vijana hao na Wakufunzi  kutoka Nangwa VTC kwa Kutoa mafunzo ya udereva bila ya kumsahau Diwani wa Kata na wote waliohusika kwa namna moja au nyingine.

Mayanja amewahakikishia vijana hao kuendelea kuwa mlezi na mshauri wao hususani katika maswala ya ajira na akatoa ahadi ya kuwapa kipaumbele kwenye nafasi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) pindi zitakapotoka.

Mayanja ameahidi na kuwapa nafasi za ulinzi  kwenye mradi mkubwa wa bomba la mafuta ambalo linapita kwenye vijiji vinne vya wilaya hiyo.

 Katika hatua nyingine Mayanja amewakaribisha SUMA JKT ambao walihudhuria hafla hiyo kwa lengo la kuwasaili vijana hao Ili  waweze kuwachukua kwa ajili ya kufanya shughuli za ulinzi na udereva.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, Kamati ya Siasa ya wilaya Ikiongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa wilaya hiyo Mathew Darema, Mbunge wa Jimbo la Hanang' Mhandisi Samwel Hayyuma ,Mbunge wa Vijana Taifa Asia Halamga, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya,wazazi,walezi, wananchi wa Kata ya  Nangwa na kata za jirani.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: