Monday, 4 October 2021

SERIKALI YATOA SHILINGI BILIONI MOJA KUTATUA KERO YA MAJI LUDEWASerikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji imeahidi kutoa shilingi Bilioni moja ili kuondoa kero ya maji kwa wananchi wilayani Ludewa.


Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema fedha hizo zitatolewa kwenye mradi wa maji wa Lifua -Manda Wilayani Ludewa ili kuwezesha usambazaji maji katika mji wa Ludewa na vijiji vinavyopitiwa na mradi."Serikali italeta shilingi bilioni moja ili kukamilisha kazi ya usambaji wa maji Ludewa mjini pia mchakato wa usambazaji maji katika vijiji vinavyopitiwa na mradi. " Alisema Naibu Waziri Mahundi.


Mheshimiwa Mahundi alisema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamilia kuwaondolea kero ya kusaka maji wanawake ambao wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji. Hivyo wataendelea kuhakikisha changamoto zote zinazokwamisha utekelezaji wa miradi ya maji zinatatuliwa.


 Amesema atamwagiza Katibu Mkuu wa wizara ya Maji kupeleka fedha hizo ndani ya wiki moja.


Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Njombe,  Mhandisi Sadick Chaka alisema wameendelea kuimarisha huduma ya usambazaji maji kwa wananchi. Hivyo kukamilika kwa mradi wa Lifua Manda kutasaidia kuondoa kero kwa ya maji katika mji wa Ludewa.


Aidha, Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamonga ameishukuri serikali kwa dhamira ya dhati ya kuondoa kero kwa wananchi.


"Mheshimiwa Naibu Waziri, huku Ludewa kilio kikubwa ambacho nimekuwa nikikutana nacho kwenye kata na vijiji ninavyotembelea ni kero ya maji. Nashukuru kwa uamzi huu utatoa ahueni kwa wananchi.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Mhe. Andrew Tsere alimweleza Naibu Waziri kuwa mradi wa Lifua-Manda umekuwa ukisubiriwa kwa hamu na wananchi ili uweze kusambaza maji kwenye vijiji vingi ili kuwaondolea changamoto wananchi.


Naibu Waziri Mhandisi Maryprisca Mahundi yuko mkoani Njombe kwa ziara ya kikazi.

No comments:

Post a Comment