Monday, 11 October 2021

SERIKALI YATAKA WATOTO KUPEWA MUDA WA KUTOSHA KUJIELEZA MAHAKAMANI.
Na Joachim Nyambo,Mbeya.


SERIKALI imeagiza watoto wanaofikishwa mahakamani kutokana na kukinzana na sheria kupewa nafasi ya kujieleza na kusikilizwa ili kuwapa fursa ya kuelezea uhalisia juu ya shitaka husika badala ya kutumia ubabe na kuwapa nafasi hiyo watu wazima pekee.


Miongoni mwa watotot ambao wamekuwa wakifikishwa kwenye mahakama hizo kutokana na kukinzana na sheria ni pamoja na walio katika umri mdogo wa chini ya miaka nane ambao wanahitaji kusikilizwa kwa makini.


Sambamba na kusikilizwa pia maafisa katika mahakama za watoto wametakiwa kutovaa mavazi yanayowatisha watoto hatua inayoweza kuwasababishiia kuingiwa na woga na kushindwa kujieleza kwa uhuru. 


Naibu Waziri wa Afya,maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto,Mwanaidi Ali Khamis alitoa maagizo hayo alipozungumza na Maafisa wanaohudumu katika Mahakama ya watoto iliyopo jijini Mbeya alipokuwa kwenye ziara ya kikazi.


Mwanaidi alisema kama ilivyo kwa watu wazima wanapofikishwa mahakamani kupewa muda wa kutosha wa kujieleza watoto wanaofikishwa pia kwenye mahakama ni muhimu wakapewa wasaa wa kutosha ili waweze kutoa maelezo kamili. 


Alisema kutopewa muda wa kutosha kujieleza kuna wanyima watoto kupata haki yao na hivyo inaweza kusababisha matokeo ya ya maamuzi kuwa sehemu nyingine ya uendelezaji wa ukatili dhidi ya watoto na hivyo kufisisha maana halisi ya uwepo wa mahakama hizo. 


Alisema pia maafisa wanaoendelea kutoa huduma kwenye mahakama hizo kuvaa mavazi yenye kutisha kunaweza kusababisha watoto kukosa haki yao kwenye hukumu kwakuwa kunaweza kuwasababishia kushindwa kujitetea na kueleza ukweli. 


“Maafisa kwenye mahakama hizi wawe tu katika mazinngira ya mwonekano wa kawaida wanapokuwa na watoto.Wasivae mavazi au kuwa na mwonekano wenye kutisha.Kuna watoto kitendo cha kuona tu askari wakiwa wamevalia magwanda wanaingia hofu.” Alisistiza 


“Au kuna wakati afisa akatumia lugha ya ukali na kumfanya mtoto anapata woga mpaka anashindwa kuwa huru.Tuwaache wajieleze kwa uhuru ili na sheria zifuate mkondo wake.” 


Kwa upande wake Kaimu Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya watoto Mbeya,Zawadi Laizer aliiomba Serikali kuiwezesha mahakama hiyo kufanya kazi kwa ufasaha ili hazipatikane kwa wakati na kusiwepo mashauri yanayochukua zaidi ya miezi sita hasa kwa watoto wanaokuja wakiwa na umri mdogo. 


Naye Afisa Ustawi wa jamii Shangwe Mshana alisema changamoto wanayokabaliana nayo katika kutekeleza Sheria ya mtoto pamoja na kanuni zake ni pamoja na kukosa mafunzo ya mara kwa mara kwa maafisa ustawi akisema bado wanalazimika ujuzi walioupata kwenye mafunzo ya zamani katika kuendesha mashauri ya watoto.


“Tunakosa mafunzo ya mara kwa mara,tunalazimika kutumia ujuzi uleule wa siku nyingi na kuna afisa ustawi mmoja hapa ambaye ni mpya hana mafunzo ya mashauri ya watoto.” 


Aliitaja changamoto nyingine kuwa ni walezi wa watoto waliokinzana na sheria na kufungulia mashauri kwenye mahakama hiyo kuacha kazi hiyo kutokana na kukosa motisha ambapo awali walianza wakiwa 10 lakini hivisasa wamesalia sita na hivyo akaomba Serikali kuwatengea bajeti walau kwaajili ya motisha ya nauli. 


No comments:

Post a Comment