Meneja wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Kanda ya Kazkazini,Patrick Shoo alizungumza na waandishi wa habari jana katika Chuo cha Mtakatifu Augustino (SAUT) mara baada ya kukabidhi tuzo ya utunzaji mzuri wa kumbukumbu wa fedha za mikopo ya wanafunzi kwa mara ya nne mfululizo.
Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Kampasi ya Arusha,Padri Charles Rufyiriza akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake mara baada chuo hicho kukabidhiwa tuzo ya kwa mara ya nne mfulululizo utunzaji mzuri wa kumbukumbu wa fedha za mikopo ya wanafunzi chuoni hapo.
Tuzo ikioneshwa.


Na Mwandishi Wetu, Arusha 


BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu nchini (HESLB) imekitunuku chuo cha Mtakatifu Augustino (SAUT) kampasi ya Arusha tuzo ya utunzaji mzuri wa kumbukumbu wa fedha za wanafunzi.

Mbali na hilo pia bodi hiyo imekitaja chuo hicho kuwa ni miongoni mwa vyuo bora nchini ambavyo vinatoa huduma rafiki kwa wanafunzi pamoja na kurejesha fedha zinazotumika kwa wakati.

Akizungumza na waandishi wa habari leo wakati akikabidhi tuzo hiyo chuoni hapo meneja wa bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kanda ya Kazkazini,Patrick Shoo alisema kwamba wamekitunuku chuo hicho tuzo hiyo kwa mara ya nne baada ya kuonekana kimefanya vizuri katika maeneo mbalimbali ya usimamizi wa fedha za mikopo ya wanafunzi.

Shoo,alisema kwamba bodi imeangalia vigezo mbalimbali kabla ya utoaji wa tuzo hiyo na kubaini kuwa chuo hicho kimefanya vizuri katika maeneo mbalimbali ambayo ni urejeshaji wa fedha za mikopo ya wanafunzi kwa wakati,huduma rafiki kwa wanafunzi na utunzaji mzuri wa kumbukumbu ya fedha za wanafunzi.

Shoo,alisema kwamba bodi ya mikopo imebadilisha mifumo ya utoaji wa mikopo ambapo serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Hassan ameongeza fedha kwenye bajeti ya mikopo inayotolewa ili kutatua changamoto mbalimbali za fedha za mikopo hiyo.

“Mifumo ya utoaji mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu imebadilishwa lakini pia Rais wetu Mama Samia ameongeza fedha hivyo sisi hatuna haja ya kuchelewesha mikopo ya wanafunzi “alisema Shoo.

Akipokea tuzo hiyo kwa niaba ya chuo hicho mkurugenzi wa chuo hicho kampasi ya Arusha,Padri Charles Rufyiriza alisema kwamba chuo chao kimejitahidi kuilinda mikopo yote inayotolewa chuoni hapo kama njia mojawapo ya kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi kuitumia mikopo yao kwa usalama.

Padri Rufyiriza alisema kwamba jumla ya wanafunzi 282 wa mwaka wa kwanza chuoni hapo tayari wameshapokea kiasi cha sh,97 milioni .

“Kwa mwaka mzima 2021/22 jumla ya sh,731 zimeshapokelewa hapa chuoni na kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza tayari asimilia 63 wa programu ya elimu,utalii na sheria wamepata mikopo “alisema Padri Rufyiriza.

Padri Rufyiriza aliishukuru bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa kutoa mikopo hiyo kwa wakati huku akisisitiza ya kwamba kwa sasa wanafunzi watasoma kwa amani.

“Tunaishukuru bodi ya mikopo kwa kutupa mikopo kwa wakati robo ya kwanza ya mikopo tayari imeshafika sasa wanafunzi watasoma kwa amani “alisisitiza Padri Rufyiriza. 

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: