Baraza la madiwani halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza limemtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuwachukulia hatua baadhi  ya watendaji  waliopewa dhamani ya kukusanya fedha kwa ajili maendeleo na kuzitafuna

Kutafunwa kwa fedha hizo zinazochangwa na wananchi kwa ajili ya maendeleo kumesababisha waanze kugoma  kuchanga.

Diwani wa  Buhama,   Petro Mbunde amesema wananchi wa kata yake wamegoma kuchanga michango ya maendeleo kutokana na watendaji wa vijiji na kata kutuhumiwa kutafuna fedha hizo.

"Watendaji wamekuwa kikwazo cha maendeleo hivyo halmashauri inatakiwa kuwawajibisha kuhusu  jambo hili ili  wananchi wawe na imani, " amesema Mbunde.

Tuhuma hizo pia zimeelekezwa kata ya Bulyahike ambako fedha za michango  zimetafunwa na watendaji kitendo kilkchowakera  wananchi.

Diwani wa Bulyaheke,   Bagetu Ngele amesema watendaji wa vijiji na  kata kwenye kata  wamekuwa kikwazo cha maendeleo na kwamba wanapaswa kuondolewa na kurudisha fedha za wananchi wanazodaiwa kutafuna.

Masumbuko Bupamba ambaye ni diwani wa  Bupandwa ameiomba halmashauri hiyo kupeleka mkaguzi wa ndani kwenye baadhi ya kata ambazo watendaji wake wanatuhumiwa kutafuna fedha za wananchi ili afanye ukaguzi na ukweli ujulikane.

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Buchosa,   Brono Sangwa  amekiri baadhi ya watendaji kulalamikiwa kutafuna fedha zinazochangwa na wananchi kwa ajili ya maendeleo.

Amemwagiza mkaguzi wa ndani kwenda  kata ya Buhama na Bulyaheke kufanya ukaguzi na kuwasilisha  taarifa  ya atakachobaini.

"Watendaji mnatuhumiwa  kutafuna fedha zinazochangwa na wananchi kwa ajili ya maendeleo lazima tuchukue hatua ili kurejesha imani kwa wananchi, " amesema Sangwa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Buchosa,  Idama Kibanzi amesema wanaotafuna fedha hizo inatakiwa wafutwe kazi.

 

H.T : Mwananchi

Share To:

Post A Comment: