Wamachinga wa soko la Samunge maarufu kama NMC jijini Arusha  wameieleza kilio chao kwa mbunge wa Jimbo la Arusha mjini Mrisho Gambo  cha kulipa ushuru wa shilingi 50 kila siku huku wanaowatoza wakiambiwa kuwa vitambulisho vya machinga  vimezikwa  na hayati Rais Dkt John Magufuli  huko Chato.


Machinga wa soko hilo wameyasema hayo Mbunge huyo alipowatembelea na kusikiliza kero zinazowakabili ambapo wakielezea kuwa kero kubwa ni ushuru wanaotozwa kila siku na wakiulizia vitambulisho vya machinga walivyokuwa wanatumia awali wanaambiwa vimezikwa Chato.


Mariam Hamis machinga katika eneo hilo alisema kuwa wananyanyasika  na ushuru huo kutokana na wao ni machinga na wanauza vitu kupitia visado na sio wafanyabiashara wakubwa hivyo  wanachokitaka ni vitambulisho kama awali kwani wana watoto  na familia zinazowategemea.


Khadija Waziri  machinga eneo Hilo alisema wananyanyaswa na wanaojiita viongozi wa machinga japo hawajawachagua kwa kuwatoza ushuru lakini pia kuwadai kila mmja shilingi 1500 ya mshahara wa walinzi  na kuwaambia umachinga ulikuwepo kipindi cha Hayati Rais Dkt Magufuli na kama wanataka kuwa machinga halisi wa wabebe makarai yao vichwani na kuzunguka nayo na sio kukaa katika soko hilo.


Neema Lomayani muuza ndizi katika soko hilo Alieleza kuwa amekuwa akilipa shilingi elfu 10000 Hadi 15000 kila siku kulingana na mzigo atakaokuwa nao jambo ambalo linamuumiza kwani hapati faida kubwa ila viongozi wa soko Hilo hawajielewi wanamuambia wanachotaka ni ushuru wa siku.


Naye Elibariki Loi mmoja kati ya walinzi Saba wa soko hilo alisema kuwa pamoja na wamachinga hao kutozwa shilingi elfu 1500 ya mshahara wa walinzi wanamalimbikizo ya mshahara wao miezi mitatu ya mwaka 2019 japo maelekezo yalishatolewa na ofisi ya mkuu wa wilaya kuwa walipwe fedha zao.


“Pamoja na changamoto hiyo kwasasa tunacheleweshewa mshahara kwa kulipwa mshahara wa mwezi iliyopita kila mwezi na sio wa mwezi husika na huyu msimamizi wa soko anavyosema walinzi wapo 9  ni  uongo kwani walinzi tupo Saba tuu na tunajuana wote,”



Aidha Mbunge wa jimbo la Arusha mjini Mrisho Gambo baada ya kusikiliza kero hizo alisema kuwa vitambulisho vya machinga bado vinatumika hivyo wanaowanyanyasa machinga na kuongea lugha zisizofaa  kuwa vitambulisho hivyo vimezikwa na hayati Rais Dkt John  Magufuli waache kwani k Rais wa awamu ya sita  Mh Rais Samia Suluhu hajavifuta vitambulisho hivyo.


 Gambo alisema kuwa machinga anatakiwa kukata kitambulisho chenye gharama ya elfu 20000 kwa mwaka na sio kulipa wa shilingi 500 ambao ni sawa na 180000 kwa mwaka hivyo atashirikisha ofisi ya mkuu wa wilaya pamoja na TAKUKURU ili kufanya uchunguzi juu ya ushuru na fedha hizo za walinzi ili kujua zinapelekwa wapi.




“Vitambulisho vya machinga vipo pale pale na wala Rais wetu wa awamu ya sita hajavifuta na alisema kuwa yeye na Hayati Rais Dkt Magufuli ni kitu kimoja   hivyo mnaoongea lugha zisizofaa msiwachonganishe wananchi na serikali ya CCM kwani hakuna aliyewatuma kufanya hivyo,”Alisema Gambo.



“Hao wamedhamiria kuwachonganisha nyie na serikali kwasababu haiwezekani wakati Jimbo lilipokuwa upinzani msinyanyasike alafu sasa hivi limerudi CCM mnakutana na mambo ya kunyang'anyana vituna kwenda kufungiwa,” Alieleza.


Sambamba na hayo pia Mbunge huyo aliwaahidi machinga  kuwa ataanxisha utaratibu wa kuangalia Ni namna gani atawasaidia akina mama kwa kuwapa mkopo  usiokuwa na riba ili kuwaokoa na mikopo inayowatesa kwa kuwa riba kubwa ambapo alisema kuwa mkopo huo utatolewa katika masoko yote matatu ambayo ni Samunge, Kilombero na soko katika soko hilo la Samunge ataanza akina mama 40 kwa kuwapa mkopo wa shilingi laki mbili.


Hata hivyo mkuu wa soko hilo alipotafutwa ili kujibu malalamiko hayo alituma ujumbe na kusema kuwa hawezi kufika katika eneo hilo kwani yupo katika ofisi za jiji la Arusha kwenye kikao.

Share To:

Post A Comment: