Afisa Vipimo Kigoma Bw. Elia Tumaini akitoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo na ufungashaji wa bidhaa kwenye maonesho ya Sido Kigoma. Afisa Vipimo Kigoma Bw. Eliud Mwakyusa akitoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo kwenye maonesho ya Sido Kigoma.

Meneja wa Wakala wa Vipimo Bw. Laurent Kabikiye akitoa elimu kuhusu ufungashaji sahihi wa bidhaa za Wajasiriamali kwenye maonesho ya SIDO Kigoma.

Afisa Vipimo Kigoma Bw. Eliud Mwakyusa akitoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo kwenye maonesho ya Sido Kigoma.

**************************

Wakala wa Vipimo Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa taasisi za Serikali zinazoshiriki katika Maonesho ya tatu ya SIDO Kitaifa ambayo yanafanyika katika Viwanja vya Umoja Kasulu Mkoani Kigoma. Meneja wa Wakala wa Vipimo Kigoma Bw. Laurent Kabikiye ameeleza kuwa, maonesho ya SIDO yamekuja kwa wakati muhafaka kwani yanatoa fursa ya Wajasiriamali wengi kukutana na taasisi mbalimbali za Serikali na kutatua changamoto zao.

Meneja Kabikiye amesema, Wajasiriamali wengi wanachangamoto katika uwekaji alama kwenye vifungashio vyao hivyo maonesho haya yamewawezesha Wakala wa Vipimo kukutana na Wajasiriamali zaidi ya 100 na kuwapa elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo na namna ya kuandika alama za Vipimo kwa usahihi ili kuongeza thamani ya bidhaa zao ziweze kushindana katika masoko ya Kimataifa.

Makosa mbalimbali yaliobainika katika ufungashaji wa bidhaa za wajasiriamali na kupatiwa ufumbuzi ni pamoja na wafungashaji wa bidhaa za asali baadhi yao wamefungasha bidhaa zao kwa ujazo wakati kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo asali ni nzito inapaswa kufungashwa kwa uzito. Hivyo, wajasiriamali wamepatiwa elimu hiyo na wameahidi kubadilisha ufungashaji wa bidhaa za asali na kufungasha kama Sheria inavyoelekeza.

Makosa mengine ambayo wajasiriamali wameelimishwa kutoyarudia kwenye vifungashio vyao ni pamoja na uandishi wa alama mbalimbali ambapo baadhi ya wajasiriamali hukosea kuandika alama hizo kama zilivyo orodheshwa; KGM, kgs, GRM, ML, lts, LTS, CM, Mm. Alama sahihi za Vipimo huandikwa kwa usahihi mfano kilogram (kg), gram (g), metre (m), centimeter (cm), milimetre (mm), mililitre (ml au Ml), litre (L au l) na siyo vinginevyo.

Kadhalika, Meneja Kabikiye amehimiza wajasiriamali kuzingatia mambo kadhaa kwenye vifungashio vyao kama kuandika jina la utambulisho wa bidhaa, kuandika jina na mahali anapofanyia biashara yake, kuweka anuani ya posta, namba ya simu na barua pepe. Vilevile, mjasiriamali anatakiwa kuainisha kiasi halisi cha bidhaa yake aliyofungasha mfano; (2 kg au 1 L) na ahakikishe anaacha nafasi moja kati ya namba na herufi mfano; 200g (Sisahihi) 200 g (Sahihi).

Wakala wa Vipimo inaendelea kutoa wito kwa Wafanyabiashara na Wajasiriamali wote kuzingatia matumizi sahihi ya Vipimo katika uuzaji na ufungashaji wa bidhaa zao ili kuhakikisha hawajipunji na hawawapunji wanunuzi wa bidhaa zao kwani kwa kufanya hivyo pande zote mbili zitaendelea kunufaika na kukuza uchumi wa biashara zao na uchumi wanchi kwa ujumla.

Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: