Na. Tito Mselem,


Kiwanda cha uzalishaji wa Nondo cha Nyakato Steel Mills Limited kilichopo Jijini Mwanza kimejipanga kufanya uwekezaji mkubwa katika uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na chuma ili kutumia fursa ya soko iliyopo kwenye Sekta ya Madini. 


Hayo ameelezwa Waziri wa Madini Doto Biteko leo Agosti 30, 2021 Jijini Dodoma alipofanya kikao baina yake na uongozi wa Kiwanda hicho. 


Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Biteko, amekishauri Kiwanda hicho kuwa, mara kitakapoanza uzalishaji wa gololi zitakazokuwa zinatumika kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa katika kusaga mawe na mchanga wa dhahabu soko litakuwepo.


“Sisi kama Wizara ya Madini tunawapongeza kwa ujenzi wa kiwanda hicho, pia tunawapa baraka kwa kuamua kuanza kuzalisha gololi hapa nchini, hivyo niwahakikishie kwamba soko lipo lakini lazima muhakikishe mnazalisha bidhaa zenye ubora mkubwa na ziwe ndizo zinazo tumika katika migodi midogo, ya kati na mikubwa,” amesema Waziri Biteko.


“Kama Kiwanda kitakuwepo chenye kuzalisha bidhaa bora za migodi, hatutaruhusu gololi zitoke nje ya nchi wakati Tanzania tuna viwanda vya kuzalisha gololi, hivyo niwape moyo endeleeni soko lipo ninacho sisitiza ni ubora wake katika matumizi,” ameongeza Waziri Biteko.


Pia, imeelezwa kuwa, masoko ya bidhaa za chuma nchini yapo kwa wingi hususan katika Sekta ya Madini na Sekta ya Ujenzi ambapo wachimbaji wadogo wa kati na wakubwa hutumia gololi katika kusaga mawe na mchanga wa madini.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Nyakato Steel Mills Limited Shenan Madhani, amemuomba Waziri Biteko kutoa Baraka za Wizara ili Kampuni iendelee na ujenzi pamoja na ufungaji wa mashine ambapo amesema baada ya kipindi cha mwaka mmoja uzalishaji utakuwa umeanza.

Share To:

Post A Comment: