Wednesday, 11 August 2021

Waziri Ummy atoa maamuzi magumu eneo la ujenzi wa makao Makuu Halmashauri ya Wilaya ya Njombe

 


Na. Angela Msimbira NJOMBE


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  Mhe Ummy Mwalimu  amebariki maamuzi ya Baraza la madiwani  kuhusu ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Walaya ya Njombe  kujengwa  katika Kijiji Kidegembye Kata ya Kidegembye, Halmashauri ya wilaya Njombe, Mkoani Njombe.


Akiongea na Viongozi wa Mkoa wa Njombe, Wilaya, Baraza la Madiwani na Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Waziri Ummy amesema amebariki maamuzi hayo kufuatia mvutano wa muda mrefu uliokuwepo wa eneo la ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri hiyo ambao umedumu tangu mwaka 2019.


Waziri Ummy amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe  kuhakikisha ujenzi unaanza mara moja kwa kuwa fedha zaidi ya shilingi milioni 900 zimetolewa na Serikali hivyo kazi ya ujenzi iendelee bila kuchelwa.


Waziri Ummy amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Njombe kunaza taratibu za kuomba fedha shilingi bilioni moja ambazo zimetengwa na Serikali katika mwaka wa fedha 2021/22 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi. 


Ameendelea kusema kuwa kwa sasa mjadala kuhusu ujenzi wa Makao Mkuu  umefungwa kinachotakiwa ni kujenga mahusiano mazuri katika kutekeleza  miradi ya maendeleo  kwa kuwataka madiwani kusimamia ujenzi huo ili uweze kukamilika kwa wakati.


Amemuagiza Afisa Mipango Miji wa Halmashauri  wa Wilaya kuhakikisha wanapanga  mpango wa kabambe wa eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu  ili iwe kama “satellite City”


Vilevile amewaagiza Halmashauri hiyo  kuhakikisha wanabuni mkakati utakaoifanya Hospitali ya Matembwe inafanyakazi  ya kutoa huduma za afya kwa wananchi


Aidha amewataka baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kusimamia ukusanyaji ya mapato ya ndani ya Halmashauri na kuhakikisha yanatekeleza kutatua kero za wananchi na kuwataka wakuu wa Idara kuhakikisha wanatenga asilimia 40 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment