Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Asimwe Rwiguza (kulia) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Juma Irando (katikati) pamoja na Katibu wa Chama cha Ushirika cha Wanawake, Nronga, Hellen Ussiri kwa pamoja wakinywa maziwa ikiwa ni ishara ya kuzindua Awamu ya Pili ya Unywaji wa maziwa Shuleni katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro jana.
Msajili wa Bodi ya Maziwa Dkt.George Msalya akizungumzia maendeleo ya tasnia ya maziwa kwenye uzinduzi huo.
    Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Asimwe Rwiguza akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Mmoja wa Maafisa wa Chama cha Ushirika cha Wanawake Nronga akigawa maziwa kwa Wanafunzi.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Asimwe Rwiguza (kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa majokofu kwa wafanyabiashara.


Na Mbaraka Kambona, Kilimanjaro


WAZAZI nchini wamehimizwa kuweka mkazo katika kuwapatia watoto wao lishe bora ikiwemo kuhakikisha wanakunywa maziwa kila wakati ili kuwafanya wawe na afya nzuri itakayowasaidia kufanya vizuri katika masomo yao. 

Rai hiyo ilitolewa na Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Asimwe Rwiguza wakati akizindua Awamu ya Pili ya Kampeni ya Unywaji Maziwa Shuleni uliyofanyika Mkoani Kilimanjaro Agosti 27, 2021.

Wakati akizindua kampeni hiyo Dkt. Rwiguza alisema kuwa jukumu la lishe lipo mikononi mwa wazazi hivyo ni muhimu wakajitahidi kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kugharamia lishe ya watoto  wao.

"Natoa wito kwa wazazi wote nchini kuona umuhimu wa kuwapa maziwa watoto,  faida za unywaji wa maziwa kwa watoto zinafahamika sitaki kuzirudia hapa, maziwa yatawajenga, watakuwa na akili na kuwasaidia kufanya vizuri katika masomo yao," alisema Dkt. Rwiguza.

Aliongeza kuwa uzinduzi huo wa awamu ya pili uwe chachu kwa jamii kuhakikisha watoto wao wanakunywa maziwa ya kutosha na zile changamoto zilizoonekana wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika awamu ya kwanza zishughulikiwe ili mafanikio yaweze kupatikana.

Naye,  Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dkt. George Msalya alisema kuwa kufuatia uzinduzi wa kampeni hiyo ni muhimu sasa kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika uchakataji wa maziwa ili kufanya maziwa hayo kupatikana kwa wingi na wakati wote hatua ambayo itawawezesha wawekezaji  kukuza uchumi wao na wa nchi kwa ujumla.

"Maziwa yanayoingia katika mfumo rasmi wa uchakataji katika Viwanda vyetu ni chini ya asilimia 3 ya maziwa yote yanayozalishwa hapa nchini, hiyo ni asilimia ndogo ukilinganisha na nchi za wenzetu, hivyo ni muhimu kuhamasisha wawekezaji ili kukuza tasnia hii ya maziwa nchini," alisema Dkt. Msalya.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Ushirika cha Wanawake, Nronga, kinachojishughulisha na uchakataji wa Maziwa Mkoani Kilimanjaro, Hellen Ussiri alisema kuwa baada ya Serikali kutoa tamko la uhamasishaji wa unywaji wa maziwa shule bado kumekuwa na mwamko mdogo hivyo Chama hicho kimefanya jitihada za kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha unywaji wa maziwa shuleni.

"Kiwanda cha Nronga kitasambaza maziwa kwa shule 10  za msingi zilizopo katika Wilaya ya Hai zenye jumla ya Wanafunzi 6151 ili kuendelea kutoa hamasa ya Unywaji wa maziwa kwa watoto," alisema Ussiri.

Aidha, alitoa rai kwa wadau mbalimbali wa biashara  pamoja na wazazi kwa ujumla kuunga mkono juhudi hizo ili walau adhma ya kuwapatia watoto wa shule maziwa mara mbili kwa wiki iweze kufanikiwa. 

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: