Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa ( mwenye tai nyekundu) kushoto mwenye suti ya bluu ni Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe kulia ni Waziri wa Habari, Mhe. Innocent Bashungwa wakijadili mambo mbalimbali yanayohusu michezo

 
 Na John Mapepele- WHUSM


Na John Mapepele- WHUSM

Shirikisho la Mpira wa Miguu wa Barani Afrika (CAF) limepongeza mikakati inayofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza michezo hususan Soka, ambapo wiki ijayo atapokea kombe la CECAFA 2021 la vijana wenye umri chini ya miaka 23.

Hayo yameelezwa na Rais wa CAF, Dkt.  Patrice Motsepe leo, Agosti 13, 2021 wakati alipokutana na Viongozi Wakuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Shirikisho la Soka nchini na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa ambapo amesema timu ya taifa ya Tanzania ina uwezo wa kuwa timu bingwa barani Afrika kutokana na umahiri iliyonayo sasa.

Aidha ameipongeza Tanzania kuwa nchi ya kuigwa kutokana na wananchi wake wengi kupenda michezo na hasa panapokuwa na mechi zinazowakutanisha vilabu vikubwa nchini kwa vile zinawaleta mashabiki hata kutoka nchi Jirani.

Ameisihi Serikali kuwa na mpango madhubuti wa kupata maeneo ya kufanyia mazoezi, viwanja bora na  kuandaa  vijana kuanzia  umri mdogo, kuwa na taasisi  za Serikali na binafsi ya  kufundisha soka, na  makocha  ili kuwa na wachezaji wa kimataifa.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali imeanza kuboresha michezo nchini chini ya mpango unaohusisha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo mpango huo unalenga kuibua vipaji vya vijana kupitia mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA, Vyuo Vikuu na Vyuo vya kati

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa ametaja miongoni mwa jitihada zilizolivutia Shirikisho hilo zinachukuliwa na Serikali katika kuendeleza michezo nchini kuwa ni pamoja na kuondolewa VAT kwenye nyasi bandia ili kuboresha miundombinu ya michezo nchini, kutunisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo unaosimamiwa na Baraza la Michezo nchini (BMT) na mkakati wa kurudisha uhai wa michezo katika Shule za Msingi (UMITASHUMTA) pamoja na Shule za Sekondari (UMISSETA).     

Waziri Bashungwa amemshukuru Mhe. Waziri Mkuu kwa kuongoza  vizuri majadiliano  baina ya Serikali na Rais huyo wa CAF ambapo amefafanua kuwa Serikali imejipanga vizuri  kutumia  michezo kama  mkakati wa  kuendeleza utalii nchini. 
 
Akitolea mfano amesema katika Mkutano Mkuu wa CAF unatarajiwa kufanyika nchini na kuwashirikisha Marais 54 wa Mpira katika nchi mbalimbali Barani Afrika na ujumbe wao utaleta faida kwenye sekta ya utalii kwa kuwa baada ya mkutano watapata fursa ya kutembelea Hifadhi za Taifa na maeneo mengine ya yenye vivutio vya utalii hapa nchini.

Ujumbe wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na michezo katika majadiliano hayo uliongozwa na Waziri mwenye dhamana ya Wizara hiyo, Mhe. Innocent Bashungwa, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Ally Possi na Rais wa Shirikisho la Soka Nchini Tanzania Wallace Karia.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: