Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza na wadau wa sekta ya uvuvi wa mkoa wa Kagera (hawapo pichani) ambapo amewaeleza kuwa wizara itafanya mapitio ya sheria na kanuni za uvuvi ili ziweze kuendana na mazingira ya sasa. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Mmoja ya wadau wa sekta ya uvuvi mkoani Kagera, Bw. Pancras Mtungireli akitoa maoni yao kuhusu maendeleo ya sekta ya uvuvi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi (hayupo pichani) kwenye kikao cha wadau hao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

...............................................................................

Sekta ya Uvuvi imepanga kufanya mapitio ya baadhi ya sheria na kanuni za uvuvi ili ziweze kuendana na mazingira ya sasa.

Haya yamesemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati alipozungumza na wadau wa sekta ya uvuvi wa mkoa wa Kagera kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Waziri Ndaki alisema kuwa kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wadau kuwa baadhi ya sheria na kanuni za uvuvi zimekuwa kikwazo katika utekelezaji wa shughuli zao. Hivyo wizara imeona ni muda muafaka kufanya mapitio ya baadhi ya sheria na kanuni hizo ili ziendane na mazingira ya sasa na kutokuwa kikwazo katika ufanyaji wa shughuli za uvuvi.

Lakini pamoja na mapitio hayo ya sheria na kanuni, wadau wa sekta ya uvuvi wametakiwa kuhakikisha wanafuata taratibu zote zilizopo katika utekelezaji wa shughuli zao za uvuvi na sio kusubiri mpaka wafuatiliwe. Aidha Waziri Ndaki aliwasihi wadau hao kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kwenye udhibiti wa uvuvi haramu kwani bila kufanya hivyo samaki wataisha majini na wao itawalazimu kutafuta shughuli nyingine za kufanya.

Vilevile kwa upande wa wataalam wametakiwa kuendelea kuwaelimisha wavuvi kutumia mbinu bora za uvuvi ili waondokane na uvuvi haramu. Aidha, amewaonya wataalam kutojihusisha na vitendo vya uvuvi haramu kwani endapo watabainika watachukuliwa hatua. Pia amewataka wataalam kuendelea kuwaelimisha wavuvi kuhusu suala la ufugaji wa samaki kwenye vizimba.

Waziri Ndaki aliwaeleza wadau hao kuwa kazi wanayoifanya ya uvuvi ni halali na inatambulika kiserikali na serikali inategemea kupata mapato kutokana na shughuli za uvuvi hivyo wanatakiwa kuwa huru wakati wanapofanya shughuli zao na endapo wanakutana na changamoto ni vema wawe wanazifikisha kwenye mamlaka husika.

Pia amezishauri mamlaka za serikali za mitaa kutathmini upya tozo walizoziweka kwenye mazao ya uvuvi, biashara ya uvuvi au kwenye shughuli ya uvuvi kwani ni nyingi.

Wadau hao wa sekta ya uvuvi wa mkoa wa Kagera wamemshukuru waziri kwa kuitisha kikao hicho ambacho wameweza kutoa changamoto na maoni yao juu ya maendeleo ya sekta ya uvuvi kwani ni kitu ambacho hawajawai kutegemea kuja kukaa na waziri na kuwasikiliza.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: